To provide the best experiences, we use technologies like cookies to store and/or access device information. Consenting to these technologies will allow us to process data such as browsing behavior or unique IDs on this site. Not consenting or withdrawing consent, may adversely affect certain features and functions.
The technical storage or access is strictly necessary for the legitimate purpose of enabling the use of a specific service explicitly requested by the subscriber or user, or for the sole purpose of carrying out the transmission of a communication over an electronic communications network.
The technical storage or access is necessary for the legitimate purpose of storing preferences that are not requested by the subscriber or user.
The technical storage or access that is used exclusively for statistical purposes.
The technical storage or access that is used exclusively for anonymous statistical purposes. Without a subpoena, voluntary compliance on the part of your Internet Service Provider, or additional records from a third party, information stored or retrieved for this purpose alone cannot usually be used to identify you.
The technical storage or access is required to create user profiles to send advertising, or to track the user on a website or across several websites for similar marketing purposes.
Maneno muhimu, uhuru, amani , mtandaoni, uhuru ,amani
upendo
umoja
madaraka
uzalendo
Matarajio ya mafunzo
Mada hii itakuwezesha:
(a) kutambua msamiati wa uzalendo.
(b) kueleza umuhimu wa uzalendo.
(c) kuigiza vitendo vya kizalendo.
(d) kusoma na kujibu maswali kutokana na makala.
(e) kutunga sentensi kwa kutumia vivumishi virejeshi. (
f) • kutunga sentensi katika usemi halisi na usemi wa taarifa.
(g) kuchambua shairi. Jumuiya ya Madola
(h) kueleza maana katika methali mbalimbali.
(i) kuandika insha ya masimulizi juu ya uzalendo.
Utangulizi
Uzalendo ni hali ya mtu kuipenda nchi yake kutoka moyoni mwake kwa kuitakia mema, kuendeleza amani na utawala mwema, kujali na kupenda raia wenzake, kuitakia nchi yake ushindi na maendeleo, kutunza mazingira pamoja na kuthamini historia na tamaduni mbalimbali za nchi yake hata na kuwa tayari kuifia.
Je, wewe ni mzalendo kwa kiasi gani? Unafikiri ni kwa nini kila mtu anafaa kuwa mzalendo? Mada hii itakuwezesha kutambua msamiati na vitendo vinavyohusiana na uzalendo na kuvitumia katika matendo na mawasiliano yako ya kila siku.
Funzo a: Msamiati wa uzalendo
Stadi: Kusikiliza na kuzungumza
Shughuli 1.1: Kutambua msamiati wa uzalendo.
Katika vikundi,
1. Shirikiana katika kukariri na kuimba wimbo wa taifa katika lugha ya Kiswahili.
Ee, Uganda Mungu imarisha,
Twakupa ujao wetu,
Kwa umoja na uhuru,
Tusimame imara.
Ee, Uganda nchi huru,
Pendo juhudi twakupa,
Pamoja na majirani,
Tutaishi kwa amani.
Ee, Uganda nchi itulishayo,
Kwa jua, ardhi ya rutuba,
Tutalinda daima,
Lulu ya taji la Afrika.
2. Tambueni na kuandika katika lugha ya kawaida masuala yanayohimiza uzalendo katika wimbo.
Funzo b: Umuhimu wa uzalendo
Stadi: Kusikiliza, kuzungumza na kuandika
Shughuli 1.2: Kueleza umuhimu wa uzalendo.
Katika vikundi,
1. Someni tena kwa makini utangulizi wa mada hii na kisha mjadili na kueleza sifa za mzalendo.
2. Kwa kurejelea sifa za mzalendo mlizojadili katika (1) hapo juu, jadiliana kuhusu umuhimu wa uzalendo nchini mwako.
Funzo c: Vitendo vya kizalendo
Stadi: Kusikiliza, kuzungumza na kuandika
Shughuli 1.3: Kuigiza vitendo vya kizalendo.
Katika vikundi,
1. Tazameni picha hizi na mtaje mnachoona au kinachotendeka.
2. Ni vitendo gani mnavyofikiri vinaweza kuchukuliwa kama vya kizalendo? Tajeni vitendo visivyopungua vitano na mviigize.
Kazi mradi
Wakati wa sherehe za siku kuu ya uhuru au siku kuu ya mashujaa, kuna nyimbo mbalimbali za kizalendo ambazo huimbwa. Hata hivyo, kuna waimbaji mbalimbali ambao wamebuni nyimbo ambazo zikiimbwa, zitakufanya ujivunie kuwa Mwanauganda. Je, kuna wimbo wowote wa kizalendo unaojua au uliowahi kusikia ukiimbwa? Kwa kutumia mtandao wa intaneti, tafuteni na kusikiliza nyimbo za kizalendo mbalimbali na kisha mziimbe.
Funzo d: Ufahamu: Jinsi Uganda ilivyopata uhuru wake
Stadi: Kusoma na kuandika
Shughuli 1.4: Kusoma na kujibu maswali kutokana na ufahamu.
Katika vikundi,
1. Shirikiana katika kusoma kifungu kifuatacho na kisha mjibu maswali yanayofuata:
Tarehe tisa mwezi wa kumi mwaka elfu moja mia tisa sitini na mbili, ndiyo siku nchi ya Uganda ilipopata madaraka kutoka mikononi mwa mkoloni. Katika historia, kuna baadhi ya wazalendo waliokuwa kwenye mstari wa mbele katika harakati za kupigania uhuru.
Baadhi ya wazalendo hawa ni kama vile, Marehemu Rais, Yusuf Kironde Lule pamoja na Ignatius Kangave Musaazi. Hata hivyo, inasemekana kuwa Musaazi alifungwa jela zaidi ya mara thelathini katika harakati hizo za uhuru. Kwa hivyo, hiyo ni ishara ya uzalendo aliokuwa nao katika kupigania uhuru wa nchi yake.
Benedicto Kiwanuka pamoja na Milton Obote pia ni miongoni mwa wazalendo wengi ambao watakumbukwa daima kwa juhudi zao. Uganda ilipata uhuru chini ya uongozi wa Rais Milton Obote akiwa waziri mkuu. Uganda ni mojawapo ya nchi za jumuiya ya madola kwa sababu ilikuwa ikitawaliwa chini ya ukoloni wa nchi ya Uingereza. Mfamle wa Buganda aliyeitwa, Sir Edward Mutesa (Kabaka Mutesa II), ndiye aliyekuwa Rais wa kwanza baada ya Uhuru katika mwaka wa 1963.
2. Shirikiana katika kutafuta maneno mapya kutokana na kifungu kisha mtumie kamusi kueleza maana ya maneno hayo.
3. Pendekezeni kichwa kwa kifungu hicho.
4. Kimazungumzo, elezeni jinsi Uganda ilipata uhuru.
5. Kuna wazalendo wengi waliochangia katika harakati za kupigania uhuru wa nchi ya Uganda. Tajeni wale mnaojua.
Funzo e: Sarufi: Sentensi zenye vivumishi virejeshi na O-rejeshi
Stadi: Kusoma na kuandika
Shughuli 1.5: Kutunga sentensi kwa kutumia vivumishi virejeshi na O-rejeshi pamoja na kuzikanusha.
Katika vikundi,
1. Shirikiana katika kusoma na kuigiza mazungumzo haya;
Abwooli: Hujambo ndugu!
Mbambu: Mimi sijambo! Labda wewe?
Abwooli: Sijambo pia. Kuna habari yoyote uliyosikia kuhusu rafiki yetu Imanishimwe? Yule aliyekuwa kiranja mkuu wa shule yetu
Mbambu: Ndiyo! Nimesikia kuwa ni yeye aliyeshinda tuzo ya mzalendo bora zaidi katika kategoria ya wanafunzi.
Abwooli: Lakini najiuliza, ni kitu gani alichokifanya kikampa huo ushindi?
Mbambu: Ni mambo mengi aliyofanya. Kwa mfano, wakati ambapo alikuwa kiranja mkuu, aliongoza wanafunzi ambao walipanda miti katika kata ambamo shule yetu inapatikana. Miti hiyo waliyoipanda, imechangia pakubwa katika utunzaji wa mazingira. Aidha, mbao ambazo zinaweza kutoka katika miti hiyo, zinaweza kutumika katika utengenezaji wa fanicha mbalimbali. Kuna mambo mengine mengi ambayo yametendeka chini ya usimamizi wake.
Abwooli: Kwa hivyo, mimi ninaona tuzo hiyo aliyopata, ilimfaa. Kwa kweli, ushindi ambao unaweza kumfanya mtu ajulikane hivyo, apewe medali inayofanana hivyo, anafaa pongezi nyingi.
2. Shirikiana katika kutambua maneno mapya kutokana na mazungumzo kisha mtumie kamusi kueleza maana ya maneno hayo.
Zingatia
Mazungumzo hayo mliyosoma na kuigiza hapo juu, yametumia baadhi ya vivumishi virejeshi pamoja na O-rejeshi. Baadhi yake ni maneno ambayo yamekolezwa katika mazungumzo ya hapo juu. Vivumishi virejeshi pamoja na O-rejeshi hutumika kurejelea nomino inayozungumziwa.
3. Kwa kutumia nomino za ngeli mbalimbali, tungeni sentensi kumi kwa matumizi ya amba- na kisha mziandike tena kwa kutumia O-rejeshi katika umoja na wingi. Shirikiana pia katika kukanusha sentensi mtakazotunga.
4. Shirikiana katika kutunga sentensi kama hizo zisizopungua jozi tano kwa kutumia amba- na O-rejeshi.
Kwa mfano;
• Kiti ambacho kinaletwa hapa ni cha mwalimu.
• Kiti kinacholetwa hapa ni cha mwalimu.
5. Kwa kuzingatia ngeli mbalimbali, shirikiana katika kufanya utafiti na kutambua ukanushaji wa sentensi zenye amba- na O-rejeshi.
Ukanusahaji
Funzo f: Usemi halisi na usemi wa taarifa
Stadi: Kusoma na kuandika
Shughuli 1.6: Kutunga sentensi katika usemi halisi na usemi wa taarifa.
Katika vikundi,
1. Shirikiana katika kusoma na kujadili maana ya sentensi zifuatazo.
(a) “Nitawaona mkiwa shuleni leo.” Mwalimu aliwaambia wanafunzi.
(b)”Bendera ya taifa inauzwa shilingi ngapi?” Mama aliuliza.
(c) “Tokeni hapa nyote!” Bawabu aliamuru.
(d) “Siku kuu ya mashujaa hutokea tarehe gani?” Mgeni aliuliza.
(e) “Mimi ndiye kiranja wa darasa hili.” Atai alidai.
Zingatia :
Usemi halisi ni maneno yaliyosemwa na mtu. Maneno halisi yaliyosemwa na mtu huwekewa alama za nukuu ilihali usemi wa taarifa ni maneno yaliyosemwa na mtu fulani lakini kwa sasa, yanasimuliwa na mtu mwingine.
2. Shirikiana katika kusoma na kujadiliana kuhusu baadhi ya mabadiliko yanayotarajiwa kutokea wakati wa kuripoti taarifa au wakati wa kusema maneno yaliyosemwa tayari na mtu mwingine.
3. Shirikiana katika kusoma sentensi zifuatazo na kisha mziandike katika usemi wa taarifa.
i) “Kila mwanafunzi aangalie hapa ubaoni!” Mwalimu aliamuru.
ii) “Tutasoma Kiswahili leo baada ya chamcha.” Kiranja alitangaza.
iii) “Sherehe kuu ya siku ya uhuru itafanyika katika wilaya ya Kaabong.” Waziri mkuu alisema.
iv) “Kila mtu anipe kalamu yangu sasa hivi!” Nsamba aliamuru.
v) “Ni nani asiyekula nyama choma ya mbuzi hapa?” Acheng aliuliza.
(vi) “Kamusi ya mwalimu iko wapi?” Mwanafunzi aliuliza.
vii) “Asante Mungu kwa kuniponya ugonjwa wa korona.” Mtoto
Funzo g: Uchambuzi wa shairi
Stadi: Kusoma na kuandika
Zingatia
Ushairi ni kazi ya sanaa ambayo hutungwa kwa mpangilio wa beti na hutumia lugha ya mkato.
Shughuli 1.7: Kuchambua shairi.
Katika vikundi,
1. Shirikiana katika kufanya utafiti na kutambua aina za mashairi kutokana na idadi ya mishororo kisha mweleze maana za istilahi za kishairi zifuatazo; ubeti, mshororo, vina, mizani, vipande, ukwapi, utao, mwandamo, ukingo, mwanzo, mloto, kimalizio/kiishio, kibwagizo, maudhui
2. Fanyeni utafiti na kueleza kwa undani juu ya mambo yanayofaa kuzingatiwa wakati wa uchambuzi wa shairi.
3. Kwa kurejelea masuala muhimu yanayofaa kuzingatiwa katika uchambuzi wa shairi.
Nchi yako huwa mama, kaa hili ukijua,
Popote ukisimama, upate kuisifia,
Ndipo wengine ‘tasema, kweli tunawatambua,
Huu ndio uzalendo, kupenda taifa lako.
Kwa raia mhitaji, mwenzako kusaidia,
‘Kiita ‘siseme huji, jaribu kumusikia,
Mnyonge umfariji, uweze kumuinua,
Huu ndio uzalendo, kupenda taifa lako.
Michezo wakiicheza, na kandanda shabikia,
Uganda kuitukuza, hewani ukirukia,
Ili nguvu kuwajaza, riadha wakikimbia,
Huu ndio uzalendo, kupenda taifa lako.
Lijenge taifa lako, lipate kuendelea,
Ukifanya kazi yako, weza kuwajibikia,
Pesa zijae mfuko, uchumi uje kukua,
Huu ndio uzalendo, kupenda taifa lako.
Nafasi ukishapewa, raia kuongozea,
Chunga pesa kuibiwa, fisadi kutoingia,
Hili likizingatiwa, kote watakusifia,
Huu ndio uzalendo, kupenda taifa lako.
Ilinde rasilimali, mazingira kutunzia,
Miti ya kila mahali, mashambani kupandia,
Wafisadi siojali, kiharibu ripotia,
Huu ndio uzalendo, kupenda taifa lako.
Ubaguzi ukatae, usawa kusimamia,
Yeyote sipendelee, ukabila kusikia,
Kama kazi upatie, wahitimu ajiria,
Huu ndio uzalendo, kupenda taifa lako.
Hapa ninasimamia, haki zote dumishia,
Binadamu kutetea, kote watakutambua,
Nchi yako mbele tia, ubinafsi achia,
Huu ndio uzalendo, kupenda taifa lako.
Funzo h: Ufafanuzi wa maana katika methali mbalimbali
Stadi: Kusoma na kuandika Uzalendo
Zingatia
Methali ni tungo fupi ambazo lengo lake maalumu ni kuonya na kutoa mafunzo kwa watu katika jamii. Methali nyingi huhitaji tafakuri ili kueleweka maana yake ya ndani inayokusudiwa.
Shughuli 1.8: Kufafanua maana za methali mbalimbali.
2. Kwa kurejelea kamusi ya methali au mtandao wa intaneti, shirikiana katika kujadili na kueleza maana na matumizi ya methali zozote zisizopungua kumi.
Funzo i: Insha ya masimulizi juu ya uzalendo
Stadi: Kuandika
Shughuli 1.9: Kuandika insha.
Katika vikundi,
1. Shirikiana katika kuandika insha mkieleza juu ya sifa za kizalendo ambazo kila mwananchi na kila kiongozi anafaa kuwa nazo.
Muhtasari wa matarajio ya mada
Katika mada hii, umejifunza:
msamiati wa uzalendo.
umuhimu wa uzalendo.
vitendo vya kizalendo.
kusoma na kujibu maswali kutokana na makala.
kutunga sentensi kwa kutumia vivumishi virejeshi.
kutunga sentensi katika usemi halisi na usemi wa taarifa.
kuchambua shairi. kueleza maana za methali mbalimbali.
kuandika insha ya masimulizi
Assignment
ASSIGNMENT : Mfano wa Shughuli jumlishi: Uzalendo MARKS : 10 DURATION : 1 week, 3 days