To provide the best experiences, we use technologies like cookies to store and/or access device information. Consenting to these technologies will allow us to process data such as browsing behavior or unique IDs on this site. Not consenting or withdrawing consent, may adversely affect certain features and functions.
The technical storage or access is strictly necessary for the legitimate purpose of enabling the use of a specific service explicitly requested by the subscriber or user, or for the sole purpose of carrying out the transmission of a communication over an electronic communications network.
The technical storage or access is necessary for the legitimate purpose of storing preferences that are not requested by the subscriber or user.
The technical storage or access that is used exclusively for statistical purposes.
The technical storage or access that is used exclusively for anonymous statistical purposes. Without a subpoena, voluntary compliance on the part of your Internet Service Provider, or additional records from a third party, information stored or retrieved for this purpose alone cannot usually be used to identify you.
The technical storage or access is required to create user profiles to send advertising, or to track the user on a website or across several websites for similar marketing purposes.
Utangulizi
Wewe kama mwanajamii, una wajibu wa kujua yanayotendeka katika jamii yenu. Pia, unastahili kujua mahali muhimu katika mazingira yako. Je, ni huduma zipi zinazopatikana katika mahali muhimu mbalimbali? Je! unaweza kumwelekeza yeyote anayekwenda katika mahali muhimu kokote bila kupoteza njia? Je, wewe unachangia vipi katika kuhifadhi na kuendeleza mahali muhimu katika jamii yako? Mada hii, itakuwezesha kutambua na kutumia
msamiati unaoyohusiana na mahali muhimu, matumizi ya dira pamoja na vipengele vya lugha vilivyoteuliwa katika mawasiliano.
Funzo a. Kutambua msamiati wa mahali muhimu katika Jamii
Shughuli 1.2 Kusoma na kuandika
Katika makundi,
1. Shirikiana kusoma na kujadiliana kuhusu taarifa katika makala hii
Jamii yetu huwa ikijumuisha sehemu mbalimbali ambazo zina umuhimu mkubwa sana kati
ka maisha ya mwanadamu. Bila sehemu hizi, maisha ya mtu hayawezi kuboreka hata kamwe kwa sababu atapatwa na upungufu fulani. Hizi ni sehemu ambazo tangu jadi zimekuwepo na michango yake haiwezi ikapigiwa mifano.
Mojawapo ya sehemu hizi maalum katika jamii ni kituo cha polisi. Hili ni jengo lililojengwa kwa kusudi la kuimarisha amani katika jamii. Iwapo mtu yeyote anavunja sheria basi hupelekwa katika kituo cha polisi ili akafunguliwe mashtaka na baadaye afikishwa mahakamani kukatiwa hukumu yake. Kutokana na kuwepo kwa kituo cha polisi katika jamii, visa vibaya vya uhalifu vimeepukwa kwa viwango vikubwa.
Vile vile, kuna sehemu za kuabudia katika jamii ambapo Wakristo huenda kanisani kila Jumamosi au Jumapili kulingana na dhehebu la mwuumini husika. Nao Waislamu vile vile, huelekea misikitini kuabudu. Kwa siku angalau wao huabudu mara tano. Siku ya Ijumaa ndiyo siku rasmi ya ibada katika dini ya Kiislamu. Maeneo haya ya ibada yamekuwa na mchango mkubwa sana katika uelekezi wa sudi za wanadamu. Watu wamefunzwa kumcha Mungu na
kuwaheshimu wenzao ili duniani kuwe na amani. Vile vile, ni katika majengo haya ya ibada ambapo waumini hufunzwa kuishi maisha mema na kujiepusha na dhambi ili siku ya kiama wasielekee jahanamu kuchomwa moto wa milele.
Shule nayo ni mahali ambapo elimu hupokezwa kwa wanafunzi ili waweze kuwa na maarifa ya kuwaongoza katika maisha yao siku za baadaye. Kuna shule za chekechea, msingi, upili na taasisi za juu za elimu kama vile vyuo vya ufundi na vyuo vikuu. Taifa letu limeweza kupiga hatua mbele kimaendeleo kwa sababu watu wengi wameweza kupokea elimu kutoka katika mashule mbalimbali.
Mahakama ni mahali ambapo hukumu hutolewa kwa wale wanaovunja sheria. Hili ni eneo ambalo limesaidia sana katika kudumisha uungwana ndani ya jamii yetu. Wanaopatwa na hatia huwa wakipewa adhabu kulingana na makosa waliyoyafanya. Kwa mfano, kuna wale ambao huwa wakihukumiwa kifungo cha miezi hadi kufikia wale wanaohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.
Hatimaye, hospitali na zahanati nazo zimekuwa na wajibu mkubwa sana katika maisha ya wanadamu kwa sababu ya kuwahudumia wale wote ambao ni wagonjwa. Matibabu mbalimbali yemekuwa yakitolewa kwa wagonjwa wa aina tofauti tofauti hospitalini bila kujali umri, rangi wala jinsia ya mgonjwa. Hili limewaepusha wagonjwa wengi kufariki kutokana na maradhi ambayo yamekuwa yakiwakumba kila siku.
2. Tafuteni maneno mapya kutokana na makala hii, kisha utumie kamusi au mtandao wa intaneti kuelezea maana yake.
3. Tambua na kuandika mahali muhimu katika jamii yako.
4. Shirikiana na wenzako kukamilisha sentensi mbalimbali.
i. Taja sehemu ambayo wanafunzi hupewa elimu ………………………….……………….
ii. Mahali ambapo watu huenda kuabudia huitwaje? ………………….……………………
iii. Ni mahali papi ambapo wahalifu hupekelwa ili wahukumiwe? ………………………….
iv. Kituo cha polisi kina manufaa gani? ………………………………………………………
v. Wagonjwa hutibiwa mahali papi? …………………………………………………………
Funzo b: Kueleza umuhimu wa sehemu muhimu katika jamii
Shughuli 2.2: Kusikiliza na kuzungumza
Katika vikundi vidogo,
1. Shirikiana na wenzako kutambua na kuandika mahali muhimu katika mazingira yako, kisha elezeeni kuhusu umuhimu wa kila mahali muhimu.
Funzo c. Kujadili shughuli zinazofanyika katika mahali muhimu
Shughuli 3.2: Kuzungumza na kuandika
Kwa kurejelea mahali muhimu mbalimbali katika jamii, jadiliana na wenzako kuhusu shughuli zinzaofanyika katika mahali muhimu. Kisha ziandike shughuli hizo na kutunga angalau sentensi mbili kwa kila shughuli.
Funzo d. Kutambua sehemu za dira
Shughuli 4.2: Kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika
Katika vikundi,
1. Tambueni na kuchora sehemu za dira
2. Kwenye dira uliyochora, onyesha sehemu zote za dira
3. Elezeeni upande wa nyumbani kwenu kutoka mahali muhimu mbalimbali.
4. Andika angalau wilaya mbili kutoka pande nne za nchi ya Uganda.
Taz: Dira ni kifaa kinachoonyesha pande za dunia ambacho huwaongoza watu kutambua maeneo mbalimbali. Mielekeo hii humwongoza mtu ajue kule anakolenga kwenda. Mfano ni Kaskazini, Kusini, Katikati, Magharibi na Mashariki. Hii ndiyo mielekeo mikuu ya dira. Pia kuna ile mielekeo midogo ya dira kama Kaskazini mashariki, Kaskazini magharibi, Kusini mashariki na Kusini magharibi. Mwongozo huu wa mielekeo ya pembe za ulimwengu ni muhimu sana kila mtu kuielewa.
Funzo e: Kueleza sehemu muhimu katika jamii kwa kutumia dira.
Shughuli 5.2 Kusikiliza na kuzungumza
Katika jozi,
1. Someni na kuigiza mazungumzo haya kisha mbadilishane majukumu.
Okecho: Samahani Anyango. Je, unaweza nionyesha barabara inayoelekea benkini?
Anyango: Naam, bila shaka. Pinduka kushoto mwishoni mwa barabara hii.
Okecho: Karibu na taa zinazoelekeza watu na magari barabarani?
Anyango: Ndio. Kisha nenda hadi ufike kwenye mzunguko wa barabara hii.
Okecho: Je, baada ya mzunguko huo nifanyeje?
Anyango: Upinde mkono wa kulia wa mzunguko huo na ujiunge na barabara ya Maji Matulivu.
Okecho: Ni sawa. Nifikapo pale nitakuwa nimewasili?
Anyango: La, fuata barabara hiyo ya Maji Matulivu na benki utaiona kwa upande wa kushoto wa barabara ile.
Okecho: Asante sana dada.
Anyango: Kwa heri.
2. Tafuteni maneno mapya kutokana na mazungumzo, kisha mtumie kamusi kuelezea maana yake.
3. Mwelekeze rafiki yako wa shuleni jinsi anavyoweza kuja kukutembelea nyumbani kwenu.
Funzo f: Kusoma makala kuhusu mahali muhimu na mtumizi ya dira.
Shughuli 6.2 Kusoma na kuandika
Katika makundi,
1. Shirikiana kusoma na kujadili taarifa kutokana na makala hii.
NAPENDA JAMII YETU
Katika jamii yetu, watu wanaishi vizuri na kwa amani. Watu katika jamii hii hufanya kazi kwa bidi na kutunza mazingira yao kwa unadhifu.
Kuna mahali muhimu katika jamii yetu. Mahali huku hutusaidia sote wanajamii. Kwa mfano, kuna hospitali mbili katika jamii yetu. Hospitali moja inaitwa Kitagata na ya pili inaitwa Kabwohe. Hospitali hizi zinatusaidia sana. Wagonjwa, wanawake wajawazito na wengine wanaohitaji msaada hukimbilia hospitali hizi. Madaktari na manesi katika hospitali hizi huhudumia watu vizuri sana. Pamoja na hospitali, kuna kanisa na misikiti. Kanisa na misikiti
ni mahali muhimu katika jamii yetu. Husaidia kufariji watu na kuwapa imani ya kutokata tamaa. Kanisa na misikiti panarejelewa kama mahali patakatifu ambapo wanajamii wa jamii yetu hujifunzia maadili. Zaidi ya hayo kuna shule mbalimbali katika jamii yetu. Shule ni mahali muhimu katika jamii yetu kwa sababu zinasaidia kuelimisha wanajamii yetu na kuwafunza stadi kadhaa za kimaisha kama vile, kutafakari, kuwasiliana vizuri na kuwa wabunifu.
Isitoshe, kuna mahali kama masoko, vituo vya polisi, vyoo vya umma na kadhalika ambavyo husaidia wanajamii yetu.
Hospitali ya Kitagata iko upande wa Magharibi wa nyumbani kwetu ilhali ile ya Kabwohe iko upande wa Mashariki. Ukitoka upande wa Mbarara kuelekea Kasese, hospitali ya Kabwohe itakuwa upande wako wa kulia ambayo ni sehemu ya Mashariki. Kutoka nyumbani kwetu kwenda shuleni ninakosomea, unaelekea upande wa kaskazini mpaka unapofika kituo cha polisi. Unapofika hapo, unapinda kushoto na kuenda upande wa Magharibi ya Kaskazini.
Binamu yangu yeye anasomea katika shule ya Kibingo ambayo iko upande wa Kusini ya Magharibi kutoka kwetu. Kutoka kwetu kufika shuleni kwake, unatumia dakika ishirini pekee ukiwa unatembea kwa miguu.
2. Tafuteni maneno mapya kutokana na makala na mshirikiane kutafuta maana yake kwa kutumia kamusi.
3. Elezea ujumbe unaopata baada kusoma makala hii.
4. Kwa kuongozwa na makala uliyosoma, elezea jinsi unavyoweza kuelekeza mtu kufika kwenu.
Sarufi:
Funzo g: Kutambua na kutumia vitenzi mbalimbali katika sentensi
Shughuli 7.2 Kusoma na kuandika
Katika makundi,
1. Someni na kujadili matumizi ya vitenzi vya aina zifuatazo;
i. Vitenzi Halisi
Hivi ni vitenzi vinavyorejelea kitendo moja kwa moja. Vitenzi halisi vinapoambatanishwa na vitenzi vidogo katika sentensi, huitwa vitenzi vikuu.
k.m: soma, kula, sikiza
• Mchezaji wa riadha alirejea jana kutoka ng’ambo.
• Mama atapikia wageni.
• Fungua mlango wa jikoni.
ii. Vitenzi Visaidizi
Vitenzi visaidizi hutangulia vitenzi halisi (vitenzi vikuu) katika sentensi ili kuleta maana inayokusudiwa kulingana na wakati au hali.
k.m: -kuwa, -ngali,
• Jua lilikuwa limewaka sana mchana wote.
• Tajiri wake angali anamsumbua na mshahara.
Taz: Kitenzi ni neno linalosimamia kitendo. Kila kitenzi huwa na shina la kitenzi (sehemu ndogo zaidi ya kitenzi ambayo ndiyo huwakilisha tendo hilo). Shina la kitenzi huambatanishwa na viambishi ili kutoa maana iliyokusudiwa kama vile mtendaji, mtendewa, wakati kitendo kinafanyika na pia kauli ya kitenzi hicho.
2. Tutunga sentensi angalau tano kwa kutumia vitenzi mlivyojadili hapo juu.
3. Kwa kushirikiana na jirani yako darasani, tunga sentensi sahihi kwa kutumia vitenzi vifuatavyo.
(a) andika
(b) -kuwa
(c) endesha
(d) -ngali
(e) pika
Funzo h:
i. Kutumia vipatanishi vya nomino vya ngeli ya u-i katika sentensi
Shughuli 8.2 Kusoma na kuandika
Katika vikundi,
1. Someni na kujadili maana ya nomino zifuatazo.
UPATANISHO WA KISARUFI
NGELI YA “U-I”
Ngeli hii hujumuisha nomino ambazo zinaanza kwa ‘m-‘ kwa umoja na ‘mi-‘ kwa wingi. Kwa sarufi ya kimapokeo,ngeli imekuwa ikijulikana kama ‘m-mi’. Majina yote ya miti na mimea yamo katika ngeli hii.
MIFANO
UMOJA WINGI
Mchezo michezo
Mlima milima
Mshahara mishahara
mshipi mishipi
moto mioto
mti miti
mkate mikate
mkono mikono
mguu miguu
mfuko mifuko
mwanzo mianzo
mwisho miisho
2. Kwa kutumia kamusi, tafuteni nomino za ngeli ya u-i na mziandike katika umoja na wingi.
3. Shirikiana na wanafunzi wenzako katika kikundi kusoma na kutambua matumizi ya nomino za ngeli ya u-i katika sentensi kwa kuzingatia upatanisho wa kisarufi.
4. Tunga sentensi sahihi angalau kumi kutokana na majedwali mliyosoma hapo juu
ii.Uakifishaji
Shughuli 9.2 Kusoma na Kuandika
Katika vikundi,
1. Tungeni sentensi angalau mbili kwa kila alama ya uakifishaji.
2. Shirikiana na wenzako kuakifisha sentensi hizi.
(i) mgeni alienda sokoni na kununua viazi nyama nyanya na vitunguu
(ii) lo ni nani aliyekuumiza hivi alisema shangazi
(iii) yule mtoto anapenda kusoma kwa bidii
(iv) daktari richard anamtibu agnes
(v) anaaitwa wakabi anatoka jijini kampala
Funzo i: Kuandika insha
Shughuli 10.2 Kuandika
Katika vikundi, jadiliana na kuandika insha kuhusu mahali muhimu katika jamii yako.
Shughuli ya jumla
Mama yako ni mtumishi wa umma. Yeye ni mfanya kazi wa serikali. Amehamishwa kutoka
sehemu moja hadi nyingine. Huko alikohamishwa, amehama na familia yake.
a) Unafikiri mnafaa kujua mahali gani muhimu katika mazingira mlikokwenda wewe na familia yako?
b) Kwa kurejelea mahali muhimu katika mazingira yako, eleza sababu mbalimbali kwa nini ni muhimu kutambua mahali muhimu katika mazingira yako.
c) Kwa kuzingatia alama za uakifishaji, andika inhsa ya maelezo ukimwelezea rafiki yako unayesoma naye jinsi anavyoweza kutoka shuleni na kukutembelea nyumbani kwenu.
Muhtasari wa mada
Katika mada hii, umejifunza kuhusu,
a. Msamiati wa mahali muhimu.
b. Sehemu mbalimbali za dira.
c. Shughuli zinazofanyika katika mahali muhimu.
d. Sehemu muhimu mbalimbali kwa kutumia dira.
e. Usomaji wa makala na kujibu maswali.
f. Matumizi ya vitenzi mbalimbali katika sentensi.
g. Matumizi ya vipatanishi vya nomino katika sentensi za ngeli ya u–i.
h. Alama zote za uakifishaji katika sentensi na vifungu vya maneno.
i. Vipengele muhimu vya uandishi wa insha ya mwongozo.
j. Uandishi insha ya mwongozo.