To provide the best experiences, we use technologies like cookies to store and/or access device information. Consenting to these technologies will allow us to process data such as browsing behavior or unique IDs on this site. Not consenting or withdrawing consent, may adversely affect certain features and functions.
The technical storage or access is strictly necessary for the legitimate purpose of enabling the use of a specific service explicitly requested by the subscriber or user, or for the sole purpose of carrying out the transmission of a communication over an electronic communications network.
The technical storage or access is necessary for the legitimate purpose of storing preferences that are not requested by the subscriber or user.
The technical storage or access that is used exclusively for statistical purposes.
The technical storage or access that is used exclusively for anonymous statistical purposes. Without a subpoena, voluntary compliance on the part of your Internet Service Provider, or additional records from a third party, information stored or retrieved for this purpose alone cannot usually be used to identify you.
The technical storage or access is required to create user profiles to send advertising, or to track the user on a website or across several websites for similar marketing purposes.
LSC: MADA KUU 1.9: MICHEZO
Utangulizi
Siku hizi michezo imekuwa ya manufaa kwa nchi nyingi. Michezo hii huwa ya aina nyingi sana na yote hufurahisha watazamaji wake. Je, wewe umewahi kushiriki katika mchezo wowote? Ni mchezo upi ambao unapenda sana? Unajua vifaa vinavyotumiwa katika michezo mbalimbali? Je, unajua umuhimu wa michezo hii kwa nchi? Je, unajua namna unavyoweza kujikinga kutoka kwa ajali ukiwa unacheza? Mada hii itakuhimiza kushiriki katika michezo ili
kufurahia manufaa yake.
Funzo a: Kutaja michezo mbalimbali inayochezwa
Shughuli 1.9: Kusikiliza na kuzungumza
Katika vikundi,
1. Jadiliana juu ya michezo mbalimbali inayochezwa na kisha kila kikundi kitaje michezo kiliyojadili.
2. Igizeni namna michezo inayohusisha mbio inavyochezwa.
3. Someni na kuigiza jinsi michezo mbalimbali inavyochezwa.
Someni na kujadiliana kuhusu aina ya michezo ifuatayo
1. Mieleka: Ni mchezo ambao watu wawili hushindana nguvu kwa kupigana na kuangushana au kubiringishana.
3. Mpira wa vikapu: Ni mchezo wa mpira ambao timu mbili hushindana katika kutupa mpira kwa mikono kuuingiza katika kikapu kinachokuwa juu.
4. Voliboli – Mchezo wa timu ya watu sita unaochezwa kwa mikono kwa kupiga mpira na kuuvusha juu ya wavu ulioweka katikati ya kiwanja kuelekea timu pinzani.
5. Mpira wa pete/netiboli – Mchezo wa mpira wa mikono unaochezwa na watu saba kila upande kwenye uwanja ambao goli zake ni milingoti miwili mirefu yenye pete na nyavu.
6. Hoki – Mchezo wa mpira ambao wachezaji hucheza kwa kutumia magongo maalumu.
7. Gofu – Mchezo unaochezwa kwa kuupiga mpira mdogo kwa kingoe.
8. Naga/gori – Mchezo unaofanana na mpira wa mguu ambao wachezaji huruhusiwa kukamata mpira na kukimbia nao.
9. Chesi/saratanji/bao – Mchezo unaofanana na bao ambao huchezwa na watu wawili ambapo kila mmoja anakuwa na vipande 6 vya kucheza vinavyoweza kusogezwa juu ya ubao wenye umbo mraba kwa uelekeo tofauti.
10. Kareti – Mtindo wa upiganaji wa kijapani ambapo mpiganaji hutumia mikono na miguu.
11. Judo – Mchezo wa mieleka ambao huchezwa na watu wawiliwawili.
12. Kriketi – Mchezo unaochezwa na timu mbili ambapo kila moja inakuwa na mchezaji.
13. Mbio – mwendo wa kasi au upesi.
14. Jugwe – Mchezo wa kuvutana kwa kamba unaochezwana timu mbili zenye wachezaji kumi na wawili kila moja.
15. Msabaka – Mashindano ya mbio za farasi wanaoongozwa na wapanda farasi.
16. Sarakasi – Michezo inayofanywa kwa ustadi mkubwa ambayo huonyesha matendo ya kishujaa na ya kushangaza.
17. Mlenge – Mashidano ya kulenga shabaha kwa kutupa vijiti vinane.
18. Langalanga – Mbio za vijigari vidogo dogo.
19. Kuogelea: Mchezo wa kuogelea majini.
3. Ambatanisha picha zifuatazo na michezo mbalimbali uliyosoma hapo juu
Funzo b: Kujadili michezo na wachezaji mashuhuri wa kimataifa
Shughuli 2.9 Kusikiliza, kusoma na kuandika
Katika makundi,
1. Tazameni picha zifuatazo na kuelezea mnachona kutokana na picha hizo.
2. Ambatanisha msamiati wa michezo uliosoma hapo awali na picha hizi.
3. Katika vikundi,
Jadiliana kuhusu michezo na wachezaji mashuhuri wa kimataifa na kisha katika makundi:
a. Tajeni wachezaji mashuhuri ambao mnajua.
b. Tajeni michezo ambayo wachezaji hao hucheza.
c. Tajeni na kuigiza jinsi michezo hiyo inavyochezwa.
4. Jadiliana kujibu maswali yafuatayo;
i. Mchezo wa kushikana na kuangushana huitwa _____.
ii. Jina jingine la mchezo wa soka ni mchezo wa _____.
iii. Mchezo wa ngumi pia huitwa _____.
iv. Mchezo wa soka huwa na wachezaji wangapi kila upande?
v. Mchezo wa kuruka kwa kutumia mti huitwa?
vi. Mchezo wa watoto wa kugotanisha miguu miwili pamoja na kurukaruka kwa kwenda mbele na nyuma ni _____.
vii. Mchezo wa kuvuta kamba wa timu za watu kumi na wawili kila upande huitwa _____.
viii. Mashindano ya mbio za farasi au watu ni _____.
ix. Mchezo wa magongo uchezwao na watu wawili au wanne ambao huingiza mipira katika vishimo huitwa _____.
x. Mbio za vijigari vidogo huitwaje? _________ .
Taz: 1. Soka/kandanda/kambumbu ni mchezo unaochezwa kwa miguu na huchezwa na timu mbili zinazoshindana.
5. Someni na kujadiliana kuhusu wachezaji wafuatao
6. Kwa kuongoza na jedwali a wachezaji mashuhuri, taja wachezaji mashuhuri unaowajua wewe pamoja na michezo yao.
Funzo c: Kubainisha vifaa vinavyotumiwa katika michezo
Shughuli 3.9: Kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika
Katika vikundi,
Jadiliana kuhusu vifaa ambavyo hutumia katika michezo na kisha:
a. Kila kikundi kichore vifaa kilivyotambua
b. Kila kikundi kidhihirishe jinsi kila kifaa hutumiwa.
c. Soma na kujadiliana kuhusu mwonekano na matumizi ya vifaa vifuatayo;
Kamba, Mpira, Mbao telezi, Maleba ya kuogelea, Firimbi, Boti, Baiskeli, Pikipiki, Wanyama, Viatu, maalum, Magongo
Funzo d: Kutengeneza vifaa vya kutumia katika michezo
Shughuli 4.9: Kusikiliza na kuzungumza
Kwa kushirikiana katika jozi,
a. Kila jozi itengewe vifaa vya michezo vya kutengeneza
b. Kila jozi isimame mbele ya darasa na kuelezea jinsi vifaa vyao vinavyotengenezwa.
Funzo e: Kueleza manufaa ya michezo
Shughuli 5.9: Kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika
Katika vikundi,
Jadiliana juu ya michezo mbalimbali na kisha:
a. Tambueni manufaa ya michezo kwa jamii fulani na nchi kwa ujumla.
b. Kila kikundi kieleze manufaa ya michezo kiliyojadili.
c. Jadiliana na kusoma kuhusu manufaa ya michezo yafuatayo;
i. Huchangamsha ubongo ili ufanye kazi vizuri.
ii. Huleta afya bora
iii. Huzuia maradhi kumshambulia mtu kwa urahisi.
iv. Michezo humfanya mtu kuwa mwenye furaha kila wakati.
v. Michezo ni ajira kwa watu wengine.
vi. Inakuza ushirikiano na umoja watu wanapokuja pamoja kutazama michezo.
vii. Inaletea nchi sifa hasa wachezaji mashuhuri wanapotamba.
Funzo f. Namna ya kuepukana na ajali katika michezo.
Shughuli 6.9 Kusikiliza na kuzungumza
Katika makundi,
1. Jadiliana kuhusu michezo mbalimbali pamoja na wachezaji wake mbalimbali.
2. Ungewashauri namna gani wachezaji ili kujikinga ajali mbali mbali katika michezo.
3. Someni na kujadiliana mambo muhimu yafuatayo
i. Epukana na kufanya mambo kwa harakaharaka bila mpango.
ii. Kanuni za mkufunzi lazima zifuatwe kwa makini sana.
iii. Vaa mavazi yanayopaswa kushabihina na aina ya mchezo husika.
iv. Epukana na ulaji wa vyakula vingi sana wakati wa michezo.
v. Mazoezi ya muda kwa muda yanapaswa kufanya ii viungo vya mwili viwe sawa.
vi. Iwapo mtu anahisi dalili zote za maumivu, amwone daktari mara moja.
Funzo g. Ufahamu
Shughuli 7.9 Kusoma na kuandika
Katika makundi,
1. Someni na kujadiliana kuhusu taarifa katika makal hii.
Michezo ina faida nyingi katika katika maisha ya binadamu. Kuna aina nyingi sana ya michezo katika jamii kama vile kandanda, mpira wa pete, riadha, masumbwi na kadhalika.
Ukiwa kama mwana michezo ndani ya jamii kwanza unakuwa na afya ya kutosha katika mwili wako kutokana na mazoezi ambayo huwa unafanya mara kwa mara. Basi utakuwa mkakamavu na afya tele.
Pili, kama mwana michezo, mtu yeyote anayefanya mazoezi ni vigumu sana kupata maradhi ya mara kwa mara kutokana na mazoezi anayoyafanya. Vijidudu vingi vya maradhi humshambulia mtu ambaye ana udhaifu katika mwili wake. Kwa wale wanaofanya mazoezi, tatizo hili huwa ni nadra sana kuwapata.
Vile vile, mchezaji kila wakati huwa ni mwenye furaha. Hii ni kwa sababu michezo huwa ikimfanya mtu kupata utulivu wa kisaikolojia na hivyo basi kusahau masaibu ambayo yamekuwa yakimwandama. Ni asilimia ndogo sana ya wana michezo ambao hawana raha ikilinganishwa na wale ambao wana raha.
Michezo ni ajira. Baadhi ya wanamichezo humu duniani wamefanya michezo kuwa kazi zao kwa sababu ya malipo mazuri wanayoyapata kutokana na michezo hiyo. Kuna baadhi ya wana michezo waliowakwasi sana kwa kutokana na michezo kiwango cha kuwashtua hata viongozi maarufu wa kisiasa ulimwenguni.
Kupitia michezo, tunafunzwa kutumia mawazo na akili zetu kwa sababu katika mchezo wowote ule, lazima mchezaji awe mbunifu ndio aweze kushinda. Bila kuwaza kimaantiki, mchezaji anaweza kugonga mwamba, na hiyo iwe ndiyo mwisho wa ndoto yake maishani.
Katika hitimisho hivyo basi, michezo ina faida nyingi sana ambayo haiwezi kukadirika. Ni wajibu wa kila mtu, mdogo kwa mkubwa, awe mpenzi wa michezo ili anufaike zaidi katika maisha yake.
2. Shirikiana na wenzako kusoma na kujibu maswali yanayofuata.
i. Je, habari hii inastahili kuwa na mada ya aina gani? Pendekeza.
ii. Dondoa mifano mitatu ya michezo iliyozungumziwa katika ufahamu huu.
iii. Mtu ambaye ana udhaifu katika mwili wake hupatwa na shida gani kulingana na mwandishi?
iv. Ni ushauri upi anaotoa mwandishi katika aya ya mwisho?
v. Je, habari hii inakufunza nini?
Sarufi
Funzo h: Kutumia nomino za ngeli ya u-i
Shughuli 8.9 Kusoma na kuandika
Katika makundi,
1. Someni na kujadiliana kuhusu matumizi ya nomino za ngeli ya u-i katika sentensi.
Ngeli ya U-I
Ngeli hii hurejelewa kama ngeli ya U-I kwa sababu nomino katika ngeli hii huwakilishwa na ‘U’ katika umoja na ‘I’ katika wingi. Nomino katika ngeli hii huanza na ‘M’ katika umoja na ‘MI’ katika wingi. Katika ngeli hii, kuna majina ya mimea, miti na nomino nyingine.
Someni na kujadiliana kuhusu mifano ya nomino za ngeli hii.
Mifano ya sentensi za umoja katika ngeli ya U-I
1. Mkate huu ni mtamu.
2. Mfuko wangu ni mkubwa.
3. Mpapai ule si mrefu.
4. Mguu wake umevunjika.
Mifano ya sentensi za wingi katika ngeli ya U-I
1. Mikate hii ni mitamu.
2. Mifuko yangu si mikubwa.
3. Mipapai ile si mirefu.
4. Miguu yangu imevunjika.
2. Shirikiana katika kikundi chako kutunga sentensi sahihi katika umoja na wingi kwa kutumia nomino zifuatazo.
(a) Mkebe
(b) Mfereji
(c) Mlima
(d) Mpini
(e) Mkufu
Funzo i. Kutumia Viunganishi katika utunzi wa sentensi
Shughuli 9.9. Kusoma na kuandika
Katika makundi,
1. Shirikiana kusoma na kujadiliana kuhusu matumizi ya viunganishi katika utunzi wa sentensi.
Zingatia. Viunganishi ni maneno yanaoyotumiwa kuunganisha neno moja na lingine, fungu la maneno na lingine au sentensi na nyingine.
Mifano ya viunganishi;
1. kama
i) Utapata kazi kama utasoma Kiswahili.
ii) Mpishi atapika chakula kama atapata kuni.
2. kwa hiyo/hivyo
i) Sijapata pesa nyingi kwa hiyo sitanunua gari.
ii). Hatujalipa karo kwa hiyo hatutaenda shuleni.
3. pia
i) Wazazi pia watazungumza Kiswahili.
ii) Mimi pia nilimwona rais.
4. kwa sababu
i) Sikusoma jana kwa sababu nilikuwa mgonjwa.
ii) Hakupita mitihani kwa sababu hakusoma kwa bidii.
5. lakini
i) Nilienda shuleni lakini sikumwona mwalimu mkuu.
ii) Nguruwe huyu anakula lakini hashibi.
6. ingawa
i). Ingawa inanyesha, nitaenda shuleni.
ii). Nitajibu swali hili ingawa ni gumu.
7. kisha
i) Mbabazi alichukua ng`ombe malishoni kwanza kisha akaenda shuleni.
ii) Wanafunzi watasafisha darasa kwanza kisha waingie wasome
8. au/ ama
i) Unataka kalamu au kitabu.
ii) Ama nitakula wali au ugali.
9. ili
i) Nimekuja shuleni ili nione mwalimu wa Kiswahili.
ii) Tumesoma Kiswahili ili tupate kazi.
10. ila/isipokuwa
i) Wanafunzi wote waingie darasani ila Okello.
ii) Watu wote watalipa isipokuwa wanafunzi.
2. Shirikiana na wenzako katika kikundi kusoma na kuunganisha sententensi zifuatazo kwa kutumia viunganishi sahihi.
i. Wananchi wanapenda amani. Wananchi wanapenda usawa.
ii. Mwalimu huyu atafundisha. Atapata chaki.
iii. Nipe kalamu. Nipe karatasi.
iv. Nilitaka kumsaidia. Sikuwa na uwezo.
v. Mtu huyu anatumia pesa ovyo. Ni mwizi.
3. Jadiliana na kutunga angalau sentensi mbili kwa kila kiunganishi kutokana na vifuatavyo.
(a) Pia
(b) Ilhali
(c) Isipokuwa
(d) Licha ya
(e) kwamba
Funzo j. Kutunga sentensi katika – hali timilifu -me-
Shughuli 10.9 Kusoma na kuandika
Katika makundi,
1. Someni na kujadiliana kuhusu matumizi ya hali timilifu.
Hali hii inatumiwa kuonesha kuwa kitendo kimetimika kabla ya kutolewa kwa taarifa.
Kwa mfano;
Soma sentensi hizi kwa sauti.
1. Nimechota maji.
2. Mohamed amekula ugali.
3. Rais ameteua mawaziri.
4. Kafeero ameenda Kampala
5. Nimekamilisha zoezi.
Mtindo wa kukubali Mtindo wa kukanusha
Nimepiga kelele. Sijapiga kelele.
Amepika chakula. Hajapika chakula.
Umesafisha vyombo. Hujasafisha vyombo.
Mmekuja hapa. Hamjaja hapa.
Tumefanya kazi. Hatujafanya kazi.
Wamekunywa pombe. Hawajanywa pombe
Tanbihi:
Katika mtindo wa kukanusha, alama ya wakati-me hugeuka –ja-. Vitenzi vya silabi moja, hupoteza –ku– ya vitenzi jina katika hali ya kukanusha.
2. Shirikiana katika makundi kujibu maswali yafuatayo
a. Andika sentensi hizi katika hali ya kukanusha
i. Baba amekuja shuleni
ii. Mwalimu amefundusha leo.
iii. Leo tumekula chakula.
iv. Nimepata fedha zangu.
v. Wanafunzi wamepita mitihani yao.
Funzo k. Kuandika Insha
Shughuli 11. 9 Kuandika
Katika makundi yenu madogo, shirikiana kuandika insha kuhusu mchezo mnaoupendao na kisha mwasilishe kazi yenu kwa wenzenu darasani.
Shughuli ya jumla
Shuleni kwenu kuna michezo mbalimbali. Wanafunzi mblimbali hupenda kucheza michezo mbalimbali pia. Kuna televisheni ambako siku za wikiendi, wanafunzi hutazamia michezo mbalimbali ya kitaifa na ya kimataifa.
a. Elezea kuhusu michezo mbalimbali inayochezwa shuleni, jinsi inavyochezwa, vifaa vinavyotumiwa katika michezo hiyo.
b. Kwa nini unafikiri ni muhimu kushiriki katika michezo mbalimbali ya wanafunzi.
Muhtasari wa mada
Katika mada hii, umejifunza kuhusu,
a. Michezo mbalimbali.
b. Wachezaji mashuhuri wa nchini na kimataifa.
c. Vifaa vya michezo mbalimbali vya michezo
d. Manufaa ya michezo.
e. Jinsi ya kuepukana na ajali katika michezo.
f. Kusoma na kujibu maswali kutokana na makala.
g. Upatanisho wa kisarufi wa ngeli ya U–I katika sentensi.
h. Matumizi ya viunganishi.
i. Utunzi wa sentensi kwa kuzingatia wakati timilifu.
j. Ukanushaji wa sentensi za hali timilifu.
k. Hatua za uandishi wa insha.
l. Uandishi wa insha.