To provide the best experiences, we use technologies like cookies to store and/or access device information. Consenting to these technologies will allow us to process data such as browsing behavior or unique IDs on this site. Not consenting or withdrawing consent, may adversely affect certain features and functions.
The technical storage or access is strictly necessary for the legitimate purpose of enabling the use of a specific service explicitly requested by the subscriber or user, or for the sole purpose of carrying out the transmission of a communication over an electronic communications network.
The technical storage or access is necessary for the legitimate purpose of storing preferences that are not requested by the subscriber or user.
The technical storage or access that is used exclusively for statistical purposes.
The technical storage or access that is used exclusively for anonymous statistical purposes. Without a subpoena, voluntary compliance on the part of your Internet Service Provider, or additional records from a third party, information stored or retrieved for this purpose alone cannot usually be used to identify you.
The technical storage or access is required to create user profiles to send advertising, or to track the user on a website or across several websites for similar marketing purposes.
Maneno muhimu
migogoro
maridhiano
madhara
mashirika
Utatuzi wa migogoro
kumbukumbu
mgomo
kiamshakinywa
rai
vurugu
tekwa nyara
kesi ya jinai
Matarajio ya mafunzo
Mada hii itakuwezesha:
(a) kuainisha migogoro mbalimbali inayoibuka katika jamii.
(b) kufafanua chanzo cha migogoro hiyo.
(c) kujadili madhara ya migogoro.
(d) kutambua mashirika na watu mashuhuri wanaohusika katika utatuzi wa migogoro.
(e) kusoma hadithi inayohusu uwiano na maridhiano na kujibu maswali.
(f) kutambua vivumishi visisitizi na kuvitumia katika sentensi.
(g) kutumia misemo halisi katika sentensi.
(h) kutunga sentensi kwa kutumia hali ya ngali na
(i) kukata rufaa
(j) ngeli. kutambua migogoro katika hadithi. kutega na kutegua vitendawili.
(k) kueleza utaratibu wa kuandika kumbukumbu za mkutano.
(l) kuandika insha ya kumbukumbu.
Utangulizi
Umewahi kukosana na mwenzako? Umewahi kumwona yeyote anayechukiana na mwenzake? Umewahi kumwona anayechonganisha wenzake? Umewahi kushiriki katika kuwapatanisha waliokosana? Hali ya migogoro katika jamii ni mbaya sana na haifai kukubalika kwa kila namna.
Kwa hivyo, maridhiano ni muhimu ili kuleta pamoja wale waliozozana kwa ajili ya kudumisha amani, usalama na maendeleo ya jamii. Mada hii itakuwezesha kutambua aina za migogoro mbalimbali, vyanzo, athari yake na jinsi ya kuendeleza maridhiano katika jamii.
Funzo a: Migogoro mbalimbali katika jamii
Stadi: Kusikiliza na kuzungumza
Shughuli 3.1: Kutaja aina za migogoro mbalimbali katika jamii.
Katika vikundi,
1. Tazameni picha hii na kisha mjadiliane kuhusu mnachoona na kilichokuwa kinatendeka. Asili: Mtandaoni
2. Mtajie mwenzako migogoro mbalimbali uliyowahi kushuhudia au kusikia katika jamii au nchi yako.
Funzo b: Chanzo cha migogoro
Stadi: Kusikiliza na kuzungumza
Shughuli 3.2: Kueleza chanzo cha migogoro mbalimbali.
Katika vikundi,
Kwa kurejelea migogoro mbalimbali mliyojadili katika shughuli 3.1 ya funzo la awali, jadilini vyanzo vya migogoro mbalimbali.
Funzo c: Athari za migogoro katika jamii
Stadi: Kusoma na kuandika
Shughuli 3.3: Kujadili athari za migogoro mbalimbali katika jamii.
Katika vikundi,
1. (a) Tazameni na kutajiana mnachoona katika mchoro ufuatao. Asili: Mtandaoni
(b) Shirikiana katika kusoma na kujadili taarifa katika makala ifuatayo;
“Hatutakula ugali leo, hata maharagwe yana vijidudu! Hatutakula! Hatuli leo! Hatuli leo!” Kelele ilianzia sehemu za nyuma ya bweni. Kila mtu alianza kukusanya chake pale darasani. Walimu walitoka madarasani kimchakamchaka! Mgomo ulikuwa umepamba moto!
Wanafunzi walisikika wakinung’unika. “Hatuwezi kula maharagwe tu kila siku, walimu wanafaa kujua kwamba sisi ni watu muhimu sana hapa shuleni! Tunafaa kula nyama kila siku. Kila siku pia, kwenye kiamshakinywa, tunataka maziwa, maandazi na mayai.” “Ndiyooo!” Wengine walijibu kwa pamoja.
Kila siku, wanatuamsha asubuhi mapema sana kusoma katika hiyo baridi yote, hata usiku baada ya chajio, wanataka tusome prep, Hakuna! Hilo hatutaki. Kila jioni tunafaa kutazama filamu na wasiotaka kutazama filamu waende walale!” “Ndiyooo!” Wengine walijibu. “Tunafaa kutazama hata mpira kila jioni na kila wikendi.” Kelele iliendelea kukaribia.
Mwalimu mkuu pamoja na walimu, walitoka nje ili kutuliza na kuzungumza na wanafunzi. Waliwarai kunyamaza na kusema yote waliyotaka ili wajadiliane juu ya suluhisho. “Weewe! Wewe, acha wewe! Waah!” Kelele iliendelea. Huko nyuma, baadhi ya wanafunzi watukutu walianza kurusha mawe kwa walimu. Walimu pamoja na mwalimu mkuu, waliingia ofisini na kupigia polisi simu.
Wanafunzi waliendeleza vurugu pale shuleni, walianza kuvunja vioo vya madirisha, walivunja madawati, walibeba na kukimbia na meza huku na huku. Madawati, viti na vijimeza vilirushwa nje, Walichanachana vitabu na karatasi kote madarasani hadi uani, waliimba nyimbo na kupiga makelele. Kuna baadhi ya wasichana waliokwenda jikoni na kutimua wapishi wote!
Walikula ugali wote fyu! Wavulana pia walikuja wakala mabaki ya ugali na maharagwe yote. Hata walikunywa mchuzi wa maharagwe na kukomba sufuria. Wengine walikuja mbio jikoni ingawa hawakupata chakula chochote! Mimi nilikuwa nimejificha ndani ya ugo wa shule na rafiki zangu watatu. Baadhi yetu hatukutaka kushiriki katika kufanya fujo.
“Buuuuummm!!!! Buuuuummm!!!! ………. Milipuko mikubwa ilisikika kutoka kila upande, nje na ndani ya shule! Ilikuwa ni milipuko ya mioshi ya kutoa machozi. Wanafunzi walianza kukimbia huku na huku wakitafuta maji ya kunawa nyusoni, wengi waliambulia patupu bila kupata hata tone la maji. Machozi yaliwatiririka tiriri! Wengine hawakuweza kuzuia makamasi kutotiririka njia mbilimbili huku wakitetemeka. Kumbe, askari polisi wanaozuia vurugu walikuwa wameshazingira shule nzima. Hakuna mwanafunzi aliyefaulu kutoroka. Sote tulitekwa nyara na kukusanywa katika sehemu moja. Magari ya polisi yenye ving’ora yalikuwa yakiingia shuleni kwa kasi msururuni! Haya yaliongeza hofu kwa kila mwanafunzi! Kila mmoja alikuwa ameanza kukana kuwa yeye hakushiriki katika mgomo huo. Mwalimu mkuu pamoja na walimu walikuwa pale pia.
Mwalimu mkuu aliwakumbusha wanafunzi jinsi alivyowaita ili wazungumze na kuwapa fursa ya kuwasilisha malalamishi yao. Aliwalaumu pia kwa kukataa kumsikiliza na badala yake wakaanza kurusha mawe yaliyovunja kila kitu pale. “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.” Alisema hilo litakuwa somo kwa kila mmoja, kwamba migogoro haifai kutatuliwa kwa fujo na vurugu kama hiyo. Aliwaelezea kwamba, ni vizuri kuwasilisha malalamishi yao wao wenyewe au kupitia viongozi wao ili wayajadili. Aliwambia kwamba hiyo kesi yao ilikuwa inamzidi. Polisi ndio wangeamua.
Kamanda wa polisi aliamuru! “Haya! Wawili wawili! Mtaingia katika basi ya shule, watakaobaki, mtabebwa na magari ya polisi. Lazima mpelekwe na polisi. Hii si kesi ya shule. Uharibifu mkubwa wa mali hii yote, ni kesi mahakamani kusomewa mashtaka yenu. Sasa, hii ni kesi ya kushughulikiwa ya jinai.” Zaidi ya wanafunzi mia moja walipelekwa mahakamani. Ilibainika kwamba wanafunzi mia tatu ndio hawakushiriki katika mgomo huo. Mimi pia nilikuwa miongoni mwa hao ambao hawakushiriki.
Siku ya kusikiliza mashtaka yao mahakamani ilipofika, hakimu aliwashtaki kwa kuharibu mali ya shule, kutosikiliza walimu wao na kujaribu kuua au kuumiza watu kwa kurusha mawe kila sehemu. Wazazi wao wote waliokuwa wamehudhuria mahakama, kila mmoja alionekana akifuta machozi na kutikisa kichwa. Baadhi ya wanafunzi wafungwa pia walionekana wakitiririkwa na machozi kila wakati. Walionekana wakiwa na nyuso za kuomba msamaha lakini hawakupewa fursa hiyo. Hakimu alipiga meza akasema; “Ushahidi uliopo unatosha kuwahukumu!” Hakimu aliwahukumu kufungwa miaka miwili na kulipa faini ya shilingi milioni mbili na nusu kwa kila mwanafunzi. Kuna baadhi ya wazazi waliowaombea watoto wao dhamana lakini hawakufaulu.
Hakimu aliwaambia; “Ndiyo, ninajua dhamana ni haki ya kila mfungwa kikatiba, lakini sitairuhusu kwa sababu, wanafunzi hawa waliharibu mali ya shule. Aidha, sababu ya malalamishi waliyokuwa nayo haina maana. Kwa mfano, walianza mgomo wakiimba kwamba hawakutaka kula siku hiyo, walisema ugali ulikuwa mbaya sana, wakidai kwamba maharagwe yalikuwa yamejaa vijidudu. Jambo la kushangaza, ni wao wenyewe waliofukuza wapishi jikoni na kula kila kitu! Hata walikomba sufuria zote, miiko pamoja na vijiko! Kwa hivyo, sioni kwa nini mtu yeyote apewe dhamana hapa.” Mtu yeyote ana uhuru wa kukata rufaa katika siku kumi na nne kutoka leo.”
“Mimi nimekuwa bado ninatafuta namna ya kupata pesa ili nimalize kulipa karo za shule. Sasa ona haya!” “Mimi juzi meneja wa mikopo benkini alinipigia simu akinidai na kunikumbusha kulipa riba ya mkopo wangu!” Sasa huyu msichana ameniua kweli. Sisi nyumbani hata hatuna chakula”, Huyu mvulana nimekuwa nikimwambia kila siku kutojiingiza katika mambo kama haya! Amenisaliti kwa kweli! Mungu wangu, nitapata wapi pesa za kulipa ili aachiliwe huru? Mimi sina pesa, labda itanibidi niuze ardhi yangu kwanza. Ndiyo njia tu ninayoweza kutumia kupata pesa!” Mnisaidie tafadhali mtoto wangu aachiliwe! Tafadhali!” Sauti za wazazi wengi zilisikika wakinung’unika na wengine wakilia mle mahakamani.
“Naomba tusikilizane tafadhali! Oda!” Hakimu aliamuru. “Kuna ushahidi pia ambao ulipatikana kwamba kuna baadhi ya wanafunzi miongoni mwa hawa ambao ndio walikuwa viongozi na wachochezi wakuu katika mgomo huo shuleni. Kwa hivyo, tumekubaliana na bodi tawala ya shule ikiwakilishwa na mwalimu mkuu aliye hapa leo. Wanafunzi hao, mbali na kulipa faini pamoja na kufungwa jela, wamefukuzwa shuleni wasirudi pale tena. Ningeomba mwalimu mkuu asimame, atusomee majina ya wanafunzi hao.” Mwalimu
aliposimama na kujaribu kukunjua karatasi yenye majina ya waliofukuzwa kabisa shuleni, kila mwanafunzi alionekana akiomba Mungu ili jina lake lisipatikane kwenye ile karatasi. Hata wazazi walikuwa vilevile wakiomba majina ya watoto wao yasipatikane kwenye orodha ile!
2. Pendekezeni anwani mwafaka ya hadithi hii.
3. Tajeni maneno mapya kutokana na makala, kisha mtumie kamusi kutafuta na kueleza maana za maneno hayo.
4. Someni na kujibu maswali yafuatayo;
(a) Elezeni sababu mbili za wanafunzi kugoma.
(b) Hakimu alitoa mfano wa sababu gani, iliyomfanya asimkubalie mwanafunzi yeyote kupewa dhamana?
(c) Watuhumiwa walipewa adhabu gani?
(d) Tajeni madhara angalau manne ya mgogoro uliotokea shuleni.
5. Kwa kurejelea migogoro mingine yoyote, elezeni athari zisizopungua tano za migogoro hiyo.
Funzo d: Mashirika na watu mashuhuri katika utatuzi wa migogoro
Stadi: Kusikiliza, Kuzungumza, Kusoma na kuandika
Shughuli 3.4: Kutambua mashirika na watu mashuhuri wanaohusika katika utatuzi wa migogoro.
Katika vikundi,
1. Katika jamii zenu, ni watu gani wanaohusika na utatuzi wa migogoro mbalimbali.
2. Kwa kutumia mtandao wa intaneti, fanyeni utafiti na kutambua mashirika mbalimbali yanayojihusisha na utatuzi wa migogoro pamoja na kueleza dhima ya kila shirika.
Funzo e: Ufahamu: Uwiano na maridhiano
Stadi: Kusoma na kuandika
Shughuli 3.5: Kusoma hadithi inayohusu uwiano na maridhiano na kisha kujibu maswali.
Katika vikundi,
1. Shirikiana katika kusoma na kujadili taarifa katika kifungu hiki.
“Wakati huo, tulikuwa hatujawahi kusemezana neno samahani au kusema ninaomba msamaha! Huo ni msamiati ambao haukuwa kinywani mwetu. Hata kutuelezea juu ya migogoro ambayo haikuwahi kuisha kati yake na jirani hivyo, tulikuwa tunachokozana sana mara kwa mara.” Kazibwe aliendelea yake Nalongo. “Kuna wakati alikata miguu ya ngo’mbe wangu wawili eti kwa sababu walipita karibu na shamba lake la wimbi. Hapo ndipo shida ilipoanzia!”
Kazibwe na Nalongo walikuwa majirani waliozozana sana kila wakati. Hata ikiwa jirani huyu angepata tatizo lolote, jirani mwingine asingethubutu kumsaidia. Hali ya maisha yao ilitutolea mafunzo mengi sisi wengine.
Siku moja, maji ya mvua kutoka kwenye nyumba ya Kazibwe, yalikuwa yakiteremka na kupita karibu na baraza ya nyumba ya Nalongo. Nalongo alimlumba Kazibwe na kugombana naye siku nzima. Alimwambia iwapo alikuwa hawezi kutafuta njia nyingine ya maji kutoka kwenye nyumba yake, aibomoe. Nalongo hakuwa mchezo!
Baada ya mwezi mmoja, Kazibwe alikuwa amesafiri masafa ya mbali. Aliporudi, alikuta nyumba yake ilikuwa imebomolewa na watu wasiojulikana. Hata ingawa alikuwa jirani yake Nalongo, hakuthubutu kumwuliza ikiwa aliwaona waliobomoa nyumba yake. Kazibwe na familia yake waliumia sana kwa kutokuwa na makazi. Hata hivyo, alimshuku Nalongo kuwa na mkono katika shughuli ya kubomoa nyumba yake kwa sababu ya mchokozano wake wa kila siku. Walijenga kibanda kwa kutumia matete na mafunjo ili kujisetiri humo kwa muda.
Baada ya miaka miwili hivi, Kazibwe alikuwa amekwishaijengea familia yake nyumba nyingine. Hata hivyo hawakuacha kuzozana yeye na jirani yake Nalongo. Kila mara wangekuwa kwa mwenyekiti wa kijiji wakiripotiana na kutozana faini kwa sababu mbalimbali. Jumamosi moja siku ya soko, Nalongo aliacha seredani ikiwaka moto jikoni, mlango ulikuwa wazi, alikimbia sokoni kidogo kununua mboga za usiku huo. Baadhi ya mikaa kwenye seredani ilipoungua, sufuria yenye maharagwe iliangusha chini ile seredani. Mikaa yenye moto iligusa kwenye baadhi ya vitu vilivyokuwa mle jikoni.
Muda si muda, cheche za moto zilianza kuruka hewani. Kazibwe alipoona hivyo, kwa haraka alimpigia Nalongo simu. “Mteja unayempigia simu hapatikani kwa sasa. Tafadhali jaribu tena baadaye.” Simu ya Nalongo haikuwa hewani. Aliwapigia kikosi cha askari polisi wazimamoto kuja kusaidia. Hata hivyo, yeye na familia yake yote walianza kuumwagilia maji ule moto kabla ya kusambaa sana.
Ungesambaa, ungechoma jiko lile pamoja na nyumba kuu ya Nalongo. Nalongo aliwasili wakati mmoja na gari la wazimamoto, alishangaa nini kilikuwa kinatendeka. Walimwelezea jinsi Kazibwe alipokuwa amewapigia simu na vile walikuta alikuwa ashaumaliza nguvu ule moto. Wazimamoto waliongeza kumwagilia maji kidogo, moto ulipozimika kabisa, wakaenda zao.
Wanakijiji walifurahia kitendo cha Kazibwe. Nalongo alifurahi sana. Alimwomba Mwenyekiti kuitisha mkutano wa wanakijiji. Mkutanoni, Nalongo alimwomba msamaha Kazibwe mbele ya wanakijiji wote, naye Kazibwe akamsamehe. Wote wawili waliridhiana na kuamua kuishi kama ndugu. Tangu siku hiyo, Nalongo na Kazibwe wanaishi kama dada na kaka.
2. Shirikiana katika kutafuta maneno mapya katika hadithi hiyo juu na mweleze maana ya maneno hayo kwa matumizi ya kamusi au mtandao.
3. Kwa nini Kazibwe alimshuku Nalongo kuwa na mkono katika shughuli ya kubomoa nyumba yake?
4. Shida kati ya Nalongo na Kazibwe ilianzia wapi?
5. Ungekuwa Kazibwe, ungeshiriki katika kuzima moto kwa Nalongo? Toa sababu zako.
6. Elezeni maoni yenu kuhusu nini kinafaa kufanyika ili kuzuia;
i) Migomo shuleni.
ii) Migomo ya raia dhidi ya viongozi wa kitaifa.
iii) Migogoro baina ya majirani.
Funzo f: Vivumishi visisitizi
Stadi: Kusoma na kuandika
Shughuli 3.6: Kutambua vivumishi visisitizi na kuvitumia katika sentensi.
Katika vikundi,
1. Shirikiana katika kusoma, kujadili na kuigiza taarifa katika mazungumzo haya.
Wambete: Muda uu huu ninafaa kuwa nimefika kwenye kituo cha polisi. Nimepigiwa simu kuwa wananisubiri saa ii hii. Nielekeze njia ya kwenda huko tafadhali.
Nakanjako: Tafadhali fuata mtoto yuyo huyo, atakuonyesha njia inayokwenda kwenye kituo hicho cha polisi.
Wambete: Ninaona watoto wawili, nimfuate nani kati ya hawa?
Nakanjako: (Anasogea na kushika bega la mvulana mwembamba) Fuata mvulana yuyu huyu. Atakuonyesha njia itakayokufikisha kuko huko unakokwenda.
Wambete: Habari mwana?
Mvulana: Ni nzuri. Shikamoo Bw. Wambete.
Wambete: Marahaba! Wewe ni mtoto mzuri. Ni nani amekufundisha salamu hasa zizi hizi za heshima? Wanatushauri kutumia salamu zizo hizo za heshima wakati tunaposalimia watu
Mvulana: Ni wazazi wangu pamoja na walimu wangu. Wanatushauri wanaotuzidi umri.
Wambete: Sawa! Unaenda wapi?
Mvulana: (Akiashiria kwenye duka lililopakwa rangi nyekundu) Ninaenda kwenye duka lile lile lenye rangi nyekundu
Wambete: Njia itakayonipeleka kwenye kituo cha polisi ni gani?
Mvulana: Fuata ii hii, itakufikisha moja kwa moja kwenye Kituo cha polisi.
Wambete: Asante!
Mvulana: Karibu
Zingatia
Maneno yaliyokolezwa katika mazungumzo ya hapo juu, hujulikana kama vivumishi visisitizi. Hivi vinatumika kusisitiza nomino inayohusika kwa kurudiarudia kivumishi kiashiria.
2. Tumieni vivumishi visisitizi kutunga sentensi moja moja katika umoja na wingi kwa kuongozwa na viashiria vya karibu sana, mbali kidogo na mbali zaidi vya ngeli angalau tano. Kwa mfano;
Funzo g: Usemi halisi
Stadi: Kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika
Shughuli 3.7: Kutunga sentensi kwa kutumia usemi halisi katika sentensi.
1. Shirikiana katika kusoma na kujadili maana ya sentensi zifuatazo;
(a) “Sitaki mchezo hapa!” Mwalimu alimaka.
(b) “Kibiriti ni pesa ngapi?” Mteja aliuliza. Katika vikundi,
(c) “Tunaomba msamaha tafadhali.” Wanafunzi walimsihi mwalimu.
(d) “Msuluhishe migogoro yenu nje ya mahakama.” Hakimu aliwashauri wanakijiji..
(e) “Tokeni hapa nyote tafadhali!” Askari aliamuru.
(f) “Sitaenda sokoni leo.” Mama alisema.
(g) “Tafadhali ninaomba maji ya kunywa.” Mgeni aliomba.
Zingatia Usemi halisi ni maneno halisi yaliyosemwa na mtu fulani. Maneno haya huwekewa alama za nukuu.
2. Kwa kuongozwa na mifano ya sentensi mlizojadili katika (1) hapo juu, shirikiana katika kutunga angalau sentensi kumi za usemi halisi.
Funzo h: Matumizi ya ngali na ngeli katika sentensi
Stadi: Kusoma na kuandika.
Zingatia Ngali na ngeli, hudhihirisha hali ya uwezekano kwamba ikiwa tukio fulani lingetokea, lingesababisha uwezekano wa tukio lingine kutokea pia. Kwa hivyo, hakuna tukio lolote lililotokea.
Shughuli 3.8: Kutunga sentensi kwa kutumia ngali na ngeli.
Katika vikundi,
1. Shirikiana katika kusoma na kujadili maana ya sentensi hizi;
(a) Namadingo angelikuwa na mbawa, angelipaa angani kama ndege.
(b) Mwalimu angalikuja leo, tungalisoma Kiswahili.
(c) Simu ingalilia mapema, ningaliamka mapema pia.
(d) Chakula kingalitosha, tungalishiba.
(e) Duku angalisoma kwa bidii, angalipita mitihani.
2. Kwa kurejelea vitendo ambavyo havikutokea kwa sababu ya kutotimiza masharti fulani, shirikiana katika kutunga sentensi angalau tano tano kwa kutumia ngali na ngeli.
Funzo i: Kutambua migogoro katika Novela
Stadi: Kusoma na kuandika Kazi mradi
Shughuli 3.9: Kusoma na kutambua maudhui ya migogoro katika hadithi.
Katika vikundi,
Mwalimu atawapendekezea novela au hadithi yoyote iliyo na maudhui ya migogoro. Kwa mfano; Rejelea visa katika Shughuli 3.5
(i) Shirikiana katika kusoma hadithi hiyo kwa kujadili sifa za wahusika.
(ii) Jadiliana na kuandika visa vya migogoro mbalimbali vinavyopatikana katika novela au hadithi hiyo.
Funzo j: Vitendawili
Stadi: Kusikiliza, kuzungumza na kuandika
Zingatia
Vitendawili ni tungo fupi zinazoficha maana ya kitu ili kisijulikane kwa urahisi na hutumiwa kwa makusudi ya kupima ufahamu wa mtu au hadhira kuhusu mazingira yake. Anayetoa kitendawili huuliza swali lake kwa kutoa maelezo mafupi yanayorejelea umbo la kitu hicho, sauti, harufu au kukifananisha na kitu kingine. Anayejibu huhitajika kufikiria haraka na kutoa jibu. Vitendawili huwa na mianzo maalumu kulingana na jamii husika.
Shughuli 3.10: Kutega na kutegua vitendawili mbalimbali.
Kwa mfano;
Mtegaji ………………….Mteguaji
Kitendawili kitendawili! ………………………………Tega!
Nyumba yangu haina mlango ………………………………Yai
Anajihami bila silaha ………………………..Kinyonga
Katika vikundi,
1. Rejelea kamusi ya vitendawili, mtandao wa intaneti au vitabu husika vya maktabani kutambua jinsi ya kutega na kutegua vitendawili mbalimbali.
2. Kwa kutumia sifa, mazingira, maumbile, matendo, mwonekano, mwenendo au tabia ya kitu fulani, tegeana na kuandika majibu ya vitendawili visivyopungua kumi.
3. Shirikiana katika kujaza mraba ufuatao.
Kulia
1. Hujihami bila silaha
2. Mfalme amezungukwa na mbwa mwitu.
3. Mkufu wangu mrefu lakini hauvaliki shingoni.
4. Nina wasichana wangu watatu, mmoja akitoka sili.
5. Chaniandama lakini hakishikiki.
6. Nina watoto wengi, nikipiga mmoja wote hulia.
7. Nanywa supu nyama naitupa.
8. Utupacho kwake ni dhahabu.
9. Nyumba yangu haina mlango.
Chini
2. Askari mweupe amesimama kwa mguu mmoja nyikani.
10. Kondoo wangu ana nyama nje ngozi ndani.
11. Adui tumemzingira lakini hatumuwezi
12. Kuku wangu katagia miibani.
13. Huku ng’o na huko ng’o.
14. Nina shamba langu kubwa, nikilivuna mavuno hayajai kiganja.
Funzo k na l: Zingatia Insha ya kumbukumbu
Stadi: Kusoma na Kuandika
Kumbukumbu ni rekodi ya majadiliano au maafikiano ya mkutano rasmi uliofanyika kwa ajili ya kuhifadhiwa au kurejelewa baadaye. Kumbukumbu huwakumbusha wahusika kuhusu yaliyojadiliwa na kufuatilia utekelezaji wa yaliyoafikiwa.
Shughuli 3.11: Kueleza utaratibu wa kuandika kumbukumbu na kisha Katika vikundi, kuiandika.
1. Shirikiana katika kusoma na kujadili ujumbe katika mfano ufuatao wa insha ya kumbukumbu na kisha mweleze utaratibu wa kuiandika. KUMBUKUMBU ZA MKUTANO WA 2 WA CHAMA CHA USAFI NA UTUNZAJI WA MAZINGIRA (CHUUM) ULIOFANYIKA KATIKA UKUMBI WA SHULE YA UPILI YA JANGOKORO TAREHE 12 JUNI 2023, KUANZIA SAA NNE ASUBUHI. Waliohudhuria;
(i) Najjingo Sylvia – Mwenyekiti
(ii) Lubengula Yunusu – Naibu mwenyekiti
(iii) Atai Shiba – Katibu
(iv) Ojok David – Mhazini
(v) Mudondo Shifra – Mwanachama
(vi) Kansiime Ruhanga Arnold – Mwanachama
(vii) Nyabong Brian – Mwanachama
Maadhura
Awisi Kavuma – Mwanachama
Patrick Oryema – Mwanachama
Waliokosa bila udhuru;
Ruyongoyongo Abdulu – Mwanachama
Ariong Angella – Mwanachama
Waalikwa
(i) Nyakaisiki Harriet – Mlezi wa chama
(ii) Emojong John Okrut – Mwalimu mkuu
Ajenda
(i) Kufungua mkutano.
(ii) Mawasilisho ya mwenyekiti.
(iii) Kusoma na kuthibitisha kumbukumbu za mkutano wa awali.
(iv) Masuala ibuka kutokana na mawasilisho pamoja na kumbukumbu.
(v) Kujadili shughuli za chama.
(vi) Mwelekeo.
(vii) Masuala mengineyo.
(viii) Kufunga mkutano.
Kumb: 1/2 CHUUM/ 2023: Kufungua mkutano.
Mkutano ulifunguliwa kirasmi saa tatu kasorobo za asubuhi kwa maombi yaliyoongozwa na Mudondo Shifra.
Kumb: 2/2 CHUUM/ 2023: Mawasilisho ya mwenyekiti. Mwenyekiti aliwashukuru sana wanachama kwa kuzingatia muda na kuhudhuria kwa wingi. Aliwasihi pia kumsamehe kwa kuita mkutano huo kwa dharura. Aliendelea kuwashukuru kwa kuwa mfano mzuri kwa wanafunzi wenzao shuleni. Alisema hili lilidhihirishwa katika kushiriki bila kuchoka katika shughuli zote za chama shuleni pamoja na nje ya shule. Mwenyekiti aliwakaribisha na kuwatambulisha wageni waalikwa ambao alisema walikuwa tayari kuunga mkono shughuli zote za chama.
Kumb: 3/2 CHUUM/ 2023: Kusoma na kuthibitisha kumbukumbu za mkutano wa awali. Kumbukumbu za mkutano wa awali wa tarehe 12 Aprili 2023 zilisomwa na katibu na kupendekezwa na Kansime Ruhanga Arnold na kuungwa mkono na Nyabong Brian kuwa ni za kweli. Mwenyekiti na katibu waliziidhinisha kwa kutia saini.
Kumb: 4/2 CHUUM/2023: Masuala ibuka kutokana na mawasilisho na kumbukumbu za muktano wa awali. Bw. Lubengula Yunusu alishukuru mwenyekiti kwa hotuba yake nzuri na baadaye akapendekeza kuwa kila mwanakamati apewe jukumu la kuongoza shughuli fulani ili kuepukana na matatizo yaliyowakumba muhula uliokuwa umepita ya mgongano wa shughuli za chama na ratiba ya masomo shuleni.
Kumbu: 5/2 CHUUM/ 2023: Kujadili shughuli za chama.
Wanachama wote walikubaliana kuwa katika muhula huo, wajikite katika;
(i) Kuhamasisha wanafunzi wenzao na wanajamii wote kuhusu umuhimu wa kupanda miti.
(ii) Kuhamasisha wanafunzi na wanajamii kuhusu kulinda na kutunza chemichemi za maji. (iii) Kuhamasisha wanafunzi na wanajamii kuhusu uepukanaji wa ugonjwa wa malaria na wa virusi vya korona..
Kumbu: 6/2 CHUUM/ 2023: Mwelekeo.
Kamati ilikubaliana kuwa kila mwanachama aunge mkono suala la kila mwanakamati kupewa jukumu la kuongoza shughuli atakayopewa ili zimalizike katika wiki moja na wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao. Kila mwanachama aliyehudhuria, aliunga mkono hoja hiyo.
Kumbu: 7/2 CHUUM/ 2023: Masuala mengineyo.
Hakuna yeyote aliyejitokeza na suala lingine la kujadiliwa.
Kumbu: 8/2 CHUUM/ 2023: Kufunga mkutano
Mkutano ulifungwa kirasmi saa tatu na nusu baada ya maombi yaliyoongozwa na Najjingo Slyvia- Mwenyekiti. Thibitisho: Mwenyekiti Katibu Tarehe Tarehe
2. Andikeni insha ya kumbukumbu za mkutano uliotokea kutatua migogoro katika familia fulani vijijini mwenu.
Muhtasari wa matarajio ya mada
Katika mada hii, umejifunza:
migogoro mbalimbali inayoibuka katika jamii. chanzo cha migogoro hiyo. madhara ya migogoro. mashirika na watu mashuhuri wanaohusika katika utatuzi wa migogoro. kusoma hadithi inayohusu uwiano na maridhiano na kujibu maswali kutambua vivumishi visisitizi na kuvitumia katika sentensi kutumia misemo halisi katika sentensi kutunga sentensi kwa kutumia hali ya ngali na ngeli. kutambua migogoro katika hadithi kutega na kutegua vitendawili kueleza utaratibu wa kuandika kumbukumbu kuandika insha ya kumbukumbu
Assignment
ASSIGNMENT : Mfano wa Shughuli jumlishi: Migogoro na Maridhiano MARKS : 10 DURATION : 1 week, 3 days