• LOGIN
  • No products in the cart.

Mada kuu 4.5: Ngoma na Burudani

Maneno muhimu

burudani

maadhimisho

jandoni.

ngoi

Matarajio ya mafunzo

Mada hii itakuwezesha:

(a) kutambua msamiati wa ngoma mbalimbali za kitamaduni

(b) kuigiza uchezaji wa ngoma mbalimbali za kitamaduni

(c) kueleza umuhimu wa burudani katika jamii

(d) kusoma makala kuhusu burudani za kitamaduni kutunga sentensi kwa kutumia viwakilishi virejeshi na ngeli ya pa-ku-mu

(e) kubaini udogo na ukubwa wa nomino mbalimbali

(f) kujadili nyimbo za tamaduni mbalimbali na ala zake.

(g) kutambua utaratibu wa kuandika insha ya tangazo.

(h) kuandika tangazo.

Utangulizi

Ngoma ni aina ya muziki au ala ambazo hutoa shauku na burudani kwa watazamaji au wachezaji. Je, ni aina gani ya ngoma inayochezwa katika utamaduni wako? Je, ni ala zipi zinazotumika katika uchezaji wa ngoma za utamaduni wako? Ngoma ya utamaduni wako huchezwaje? Mada hii itakuwezesha kutambua msamiati unaohusiana na ngoma pamoja na burudani za tamaduni mbalimbali. Pia itakuwezesha kutambua matumizi ya msamiati wa ngoma na burudani katika uimarishaji wa mawasiliano yako ya kila siku.

Funzo a: Ngoma mbalimbali za kitamaduni

Stadi: Kusikiliza na kuzungumza

Shughuli 5.1: Kutambua ngoma mbalimbali za kitamaduni.

Katika vikundi,

1. Tazameni na kujadiliana juu ya picha zifuatazo. Tajeni jina la ngoma na burudani ya kitamaduni na jamii inayoicheza nchini Uganda.

2. Shirikiana katika kutaja aina za ngoma nyingine zinazochezwa katika jamii mbalimbali nchini Uganda.

Funzo b: Uigizaji wa ngoma za kitamaduni

Stadi: Kusikiliza na kuzungumza

Shughuli 5.2: Kuigiza ngoma mbalimbali za kitamaduni na kutaja ala zinazotumika katika kucheza ngoma hizo.

Katika vikundi,

1. Elezeni na kuigiza jinsi angalau ngoma mbili kutokana na mlizojadili katika shughuli 5.1 hapo juu zinavyochezwa.

2. Tajeni na kuambatanisha kila aina ya ngoma na ala zinazotumika katika kucheza ngoma hiyo.

Funzo c: Umuhimu wa burudani

Shughuli 3: Kusikiliza, kuzungumza na kuandika

Shughuli 5.3: Kueleza umuhimu wa burudani kwa jamii.

Katika vikundi;

1. Tambueni na kujadili umuhimu wa burudani kwa jamii.

Funzo d: Ufahamu

Stadi: Kusoma

Shughuli 5.4: Kusoma makala kuhusu burudani mbalimbali na kujibu maswali.

Katika vikundi,

1. Shirikiana katika kusoma makala ifuatayo kisha mjibu maswali yatakayofuata.

Ngoma ya Wagisu

Nilipokuwa shuleni, nilikuwa mpenzi mkuu wa ngoma na burudani za kitamaduni. Ningesikia kwamba kungekuwa na maadhimisho ya kitamaduni mahali fulani ningehakikisha kuwa nimefika huko. Nilijionea mengi kuhusu burudani katika maeneo ya Magharibi, Kusini, Mashariki na hata Kaskazini mwa Uganda.

Utajiri wa tamaduni hizi unafanya nchi ya Uganda kusifika sana kote ulimwenguni. Baadhi ya watalii hutoka Ulaya, Marekani, Asia na hata kutoka nchi nyingine za bara la Afrika huja kujionea ngoma na burudani nchini Uganda. Wengi hufurahia sana na hata wengine hushiriki katika uchezaji. Ngoma na burudani huwa ni kitulizo cha moyo.

Huweza kutuliza yeyote kisaikolojia na vilevile huletea mhusika afya njema anaposhiriki. Miongoni mwa ngoma ninazokumbuka sana ni ile ya mwaga ya Wagisu kutoka Mashariki mwa Uganda. Nakwambia sikulala licha ya safari yangu ndefu kutoka milima ya Ibanda iliyo Magharibi mwa Uganda. Nilipita Kampala na kufululiza kupitia Jinja, Iganga hadi viungani mwa Mbale ubavuni mwa mlima wa Elgon. Rafiki yangu aliyeitwa Wafula alikuwa amenialika niende kujumuika nao wakati huo wa msimu wa tohara.

Yeye mwenyewe alikuwa anatiwa jandoni. Nilikuwa nimesikia tu taarifa zao lakini sasa nilitaka kujionea macho kwa macho. Sisi tuliwaita Wagishu lakini nilipofika huko nilibaini walijiita Bamasaba. Tohara yao ilifanana na ya ndugu zao Wabukusu kutoka Kenya.

Nilimpata Wafula, akanipokea na baadaye akajumuika na vijana wengine waliocheza kwa kupiga vijiti na kengele kwa njia ya kipekee na ya kufurahisha. Waliruka juu kwa mbwembwe na hanjamu kuu. Walitarajiwa kukabiliana na ‘imbalu’ siku ambayo ingefuata. Ngoma hii ilishirikisha jamii nzima katika mikatiko na midundiko ya hali ya juu ya kumtoa nyoka pangoni. Si wanawake, si wanaume, si vijana, si wazee, si wavulana, si wasichana yaani angalau kila aliyevutiwa alijiunga na burudani huku wengine wakinengua viuno mbele na nyuma kana kwamba havikuwa vyao. Mimi pia sikuachwa nyuma. Nilijiunga nao nikasakata ile ngoma!

Baadhi ya wanaume walionekana wamebeba vijiti, rungu na matawi ya miti wakicheza kwa mviringo. Naye Ngoi aliongoza nyimbo huku kundi likiitikia kwa mkarara kwa hisia kana kwamba walishikwa na mizimu ya kwao. Nao watahiriwa waliruka kwa mdundo wa ngoma na vyombo vinginevyo. Niliambiwa kwamba vijana hawa waliotarajiwa kumkabili ngariba siku ambayo ingefuata, walikuwa wamezuru watu wa jamii yao kwa muda wa karibu majuma matatu. Walikuwa wakiwazuru kuwafahamisha na kuwapa mwaliko waje kushuhudia tohara yao.

Miongoni mwa shughuli za sherehe hii, kulikuwa na mtahiriwa huyu kuzunguka kijijini huku akipeperusha mkia wa nyani wenye madoa ya rangi nyeusi na nyeupe. Hii ilikuwa njia ya kumjasirisha asiogope kitu chochote. Jioni ya kutangulia tohara yenyewe, vijana walitarajiwa kwenda ujombani ambapo walichinjiwa ng’ombe ambaye sehemu zake zilikatwa na kuvishwa shingoni mwa watahiriwa. Nyama iliyosalia ilibebwa na kikosi kilichoandamana naye hadi nyumbani. Kila kitu kilifuata desturi kama zilivyofanywa na mwanzilishi wa ‘imbalu’ aliyeitwa Mango.

Asubuhi ilipofika, kijana na wenzake walipelekwa mtoni na kupakwa tope halafu wakarejeshwa nyumbani uchi kama walivyozaliwa. Wafula alielekea sehemu aliyotengewa huku jamii nzima ikishuhudia ujasiri wake. Alisimama kidete! Ngariba alimwendea akamtahiri. Watu walioshuhudia ujasiri wake walimpongeza kwa kuimba wakimsifu kwa kuwa mwanamume kamili. Alitarajiwa kuingia katika jando na kufundishwa mambo ya utu uzima. Baada ya hayo yote, nilirudi nyumbani kwetu Ibanda nikasimulia kuhusu burudani ya kukata na shoka niliyohudhuria. Watu walifurahia sana hasa ile video niliyorekodi. Waliitazama, wakarudia, wakaitazama, kwa kweli, iliwavutia mno. Sitaisahau siku hiyo.

Maswali:

1. Tafuteni na kueleza maana ya msamiati ufuatao kulingana na ulivyotumika

(a) maadhimisho.

(d) msimu.

(g) jando. (b)

(e) ngoi kitulizo.

(c) viungani.

(f) ngariba.

2. Msimulizi wa hadithi hii alivutiwa na ngoma na burudani tangu lini?

3. Tajeni baadhi ya maeneo ambayo msimulizi alitalii ili kushuhudia ngoma na burudani za tamaduni mbalimbali akiwa shuleni.

4. Elezeni umuhimu wa ngoma na burudani kulingana na taarifa.

5. Jadilini mambo ambayo mtahiriwa alipitia kabla ya kutahiriwa kulingana na msimulizi. gani?

6. Uimbaji wa nyimbo na upakaji wa tope kwa mtahiriwa ulikuwa na maana

7. Ni sababu gani zilizofanya msimulizi kuhudhuria tohara hii?

8. Baada ya sherehe ya tohara hii msimulizi alifanya nini?

Funzo e: Sarufi

Stadi: Kusoma na kuandika

i) Viwakilishi Virejeshi

Zingatia

Haya ni maneno ambayo hutumika kurejelea na kusimamia nomino. Umbo la amba- pamoja na O-rejeshi hutumika kurejelea nomino inayozungumziwa katika sentensi.

2. Shirikiana katika kutunga sentensi zozote mbili mbili za ukaribu, umbali kidogo na umbali zaidi kwa kuzingatia ngeli ya Pa-Ku-Mu.

Funzo f: . Udogo na Ukubwa wa nomino

Stadi: Kusoma na kuandika

Shughuli 5.7:

Katika vikundi,

1.Kubainisha udogo na ukubwa wa nomino mbalimbali. Shirikiana katika kusoma na kujadili matumizi ya nomino za udogo na ukubwa katika kutunga sentensi.

Zingatia

Udogo wa nomino hutumika kusifia au kudharau kiasi cha udogo wa nomino husika. Nomino zinapowekwa katika hali hii ya udogo, hutanguliza sauti ki- au kiji- na kwa hivyo huwa zimeingia katika ngeli ya ki-vi. Hizi hutumia upatanisho wa kisarufi wa ngeli ya ki-vi katika utunzi wa sentensi. Kwa mfano;

2. (a) Tajeni na kuigiza uimbaji wa wimbo wowote mmoja unaoimbwa katika jamii yako kutokana na shughuli mojawapo kati ya zifuatazo;

i) Sherehe za mfalme

iii) ibada

v) Kuunganisha watu

ii) tohara.

iv) Shukrani ya mavuno.

vi) vita

vii) Kubembeleza watoto.

viii) ndoa

(b) Imla Mwalimu atawasomea majina ya ala zinazotumika katika uchezaji wa ngoma mbalimbali. i) Sikilizeni kwa makini na myaandike kwa kuzingatia tahajia sahihi. ii) Shirikiana katika kueleza maana na jinsi ala hizo zinavyotumika.

Funzo h: Insha ya tangazo

Stadi: Kusoma na Kuandika

Shughuli 5.9: Kutambua utaratibu wa kuandika insha ya tangazo.

Katika vikundi,

Someni mfano wa tangazo lifuatalo na kisha mjadiliane kuhusu muundo wake.

SHULE YA UPILI YA KARUMA

SANDUKU LA POSTA 400,

KARUMA.

TANGAZO

14.07.2024

TANGAZO KUHUSU KONGAMANO LA KISWAHILI SHULENI

Tungependa kuwatangazia kwamba tutakuwa na kongamano la Kiswahili shuleni kwetu siku ya Jumatano tarehe 02.09-2020 kuanzia saa tatu kamili asubuhi. Idara ya Kiswahili imealika shule kumi kutoka pembe tofauti nchini kujumuika nasi ili kuweka mikakati ya kuimarisha Kiswahili. Kufuatia tangazo hili, tungependa kujulisha wanafunzi, walimu na wafanyakazi wote wa shule kuwa hatutakuwa na ratiba ya kawaida ya masomo kwa sababu ya kongamano hili.

Nyote mwakaribishwa kuhudhuria kongamano hili kwa vile ni shughuli rasmi ya shule. Asanteni Akkn S &ba Akello Nusaiba Mwalimu Mkuu

Funzo i: Kuandika Insha ya tangazo

Stadi: Kuandika

Shughuli 5.10: Kuandika insha ya tangazo.

Mnapanga kuandaa tamasha la burudani la kitamaduni katika shule yenu. Mkiwa vikundini, shirikiana katika kuandika tangazo la kualika watu kuja kuhudhuria tamasha hilo.

Muhtasari wa matarajio ya mada Katika mada hii, umejifunza: kutambua msamiati wa ngoma mbalimbali za kitamaduni kuigiza uchezaji wa ngoma mbalimbali za kitamaduni kueleza umuhimu wa burudani katika jamii kusoma makala kuhusu burudani za kitamaduni kutunga sentensi kwa kutumia viwakilishi virejeshi na ngeli ya pa-ku- mu kubaini udogo na ukubwa wa nomino mbalimbali kujadili nyimbo za tamaduni mbalimbali na ala zake. kutambua utaratibu wa kuandika insha ya tangazo. kuandika tangazo.

Assignment

Mfano wa Shughuli jumlishi: Ngoma na Burudani

ASSIGNMENT : Mfano wa Shughuli jumlishi: Ngoma na Burudani MARKS : 10  DURATION : 1 week, 3 days

 

Courses

Featured Downloads