• LOGIN
  • No products in the cart.

Mada kuu 4.7: Rasilimali

Maneno muhimu

mazingira

tunza

potoka kimaadili

ukaidi

tandabui za buibui

kupiga domo

kung’oa

migodi

malishoni

uchimbaji madini

Matarajio ya mafunzo

Mada hii itakuwezesha:

(a) kutambua msamiati wa madini mbalimbali. kueleza umuhimu wa rasilimali

(b) kufafanua hatua mbalimbali za kutunza mazingira.

(c) kudhihirisha upandaji wa miti ili kutunza mazingira.

(d) kusoma makala yanayohusu uharibifu wa mazingira.

(e) kutambua na kubaini ukanushaji wa vitenzi katika ngeli tofauti.

(g) kugeuza misemo na sentensi halisi kuwa za taarifa.

(h) kutaja na kuelezea istiari na tashbihi.

(i) kueleza utaratibu wa kuandika barua rasmi na wasifukazi.

(j) kuandika barua rasmi.

Utangulizi

Rasilimali Rasilimali ni mali asili au vitu muhimu vya thamani vinavyotokea katika maumbile ya ardhi ambavyo vinaweza kutumika kwa uzalishaji wa uchumi au kwa matumizi mengine yenye faida kwa jamii.

Je, ni vitu gani asilia ambavyo ni muhimu na vyenye thamani nchini mwako? Je, rasilimali hizi huchangiaje maendeleo ya taifa lako kiuchumi? Kwa hivyo, Mada hii itakuwezesha kutambua na kutumia msamiati unaohusiana na rasilimali pamoja na kutambua matumizi ya vipengele vya lugha mbalimbali ili kuimarisha mawasiliano yako ya kila siku.

Funzo a: Msamiati wa rasilimali

Stadi: Kusikiliza na kuzungumza

Shughuli 7.1: Kutambua na kutaja msamiati wa madini mbalimbali.

Katika vikundi,

1. Tazameni picha zifuatazo kisha mtaje madini mnayoona.

Rasilimali

Funzo b: Umuhimu wa rasilimali

Stadi: Kusikiliza, kuzungumza

Shughuli 7.2: Kueleza umuhimu wa rasilimali.

Katika vikundi,

1. Kwa kurejelea michoro ya rasilimali iliyojadiliwa katika shughuli 7.1 hapo juu, jadiliana kuhusu sifa na umuhimu wa rasilimali hizo.

2. Mbali na madini yaliyojadiliwa katika shughuli 7.1 hapo juu, jadiliana na kutaja rasilimali nyingine mbalimbali zinazopatikana katika mazingira yenu pamoja na umuhimu wake.

Funzo c: Utunzaji wa mazingira

Stadi: Kusikiliza, kuzungumza, kusoma na kuandika

Shughuli 7.3: Kufafanua hatua mbalimbali za kutunza mazingira.

Katika vikundi,

1. Tazameni na kulinganisha picha za rasilimali zinazoonyeshwa katika upande wa A na B ifuatavyo.

2. Jadiliana juu ya umuhimu wa kutunza rasilimali na hasara ya kuyaharibu mazingira kama ilivyojitokeza katika baadhi ya picha za hapo juu.

3. Shirikiana katika kufafanua hatua mnazoweza kuchukua kuhakikisha kwamba mazingira yanatunzwa.

Funzo d: Uhifadhi wa mazingira: Kupanda miti

Stadi: Kusikiliza na kuzungumza

Shughuli 7.4: Kupanda miti kwa ajili ya kutunza mazingira.

Kazi mradi

Mkiwa katika vikundi vyenu, shirikiana katika kupanda miche ya miti katika maeneo ya shule kwa ajili ya kutunza mazingira.

Funzo e: Ufahamu: Uharibifu wa mazingira

Stadi: Kusoma na kuandika

Shughuli 7.5: Kusoma makala ya uharibifu wa mazingira na kujibu maswali.

Katika vikundi,

1. Shirikiana katika kusoma kifungu kifuatacho kisha mjibu maswali yatakayofuata.

Mazingira ya shule

Mazingira ya shule ni muhimu sana kwa mwanafunzi. Mwanafunzi humaliza muda mwingi katika maisha yake ya masomo shuleni. Kwa hivyo, anastahili kuhakikisha anayatunza mazingira ya shule yawe safi. Hata hivyo kuna wanafunzi ambao wamepotoka kimaadili. Wao huchafua mazingira ya shule. Ukaidi huu hufanya wanafunzi hawa waharibifu kukosana na walimu wao hata viranja ambao wamepewa majukumu ya kusimamia wanafunzi wenzao.

Darasa ni sehemu muhimu ambamo wanafunzi hukutana na walimu kwa ajili ya masomo. Baadhi ya wanafunzi wasiojali wamewahi kuchafua darasa kwa kutupa karatasi, vitabu, vichongeo, kalamu na vifaa vyao vya kusomea darasani bila kujali. Wengine hubeba mavumbi kutoka nje wakati wa kiangazi na hata rundo la matope wakati wa mvua kwa viatu vyao na kuharibu kabisa sakafu ya darasa. Si ajabu hata wengine wakapangusia mikono yao michafu kwenye ukuta na kuufanya kuonekana vibaya. Mbali na kuchafua darasa kwa njia hii, wanafunzi wengine huwa wavivu ambapo wakiambiwa kufagia darasa, wao hukataa. Aidha, wengine hawajali tandabui za buibui kwenye kuta na paa darasani. Hii ni tabia ya kuudhi sana.

Upigaji wa kelele darasani pia ni miongoni mwa njia za kuchafua mazingira. Wanafunzi wenye mazoea ya kupiga domo hutatiza wanafunzi wenzao wenye nia ya kutia bidii ya mchwa masomoni ili kufaulu katika mitihani. Baadhi ya wale wanaopiga kelele darasani huwa wamekata tamaa maishani ambapo wao hutaka kuwaharibia wenzao masomo. Kwa hivyo, ni wajibu wa kila mwanafunzi darasani kujali mwenzake pasipo kufanya kelele kwa sababu ya ubinafsi wake wa kutaka kujionyesha mbabe. Kunao wanafunzi ambao pia huharibu baadhi ya mimea kama vile maua au miti iliyopandwa katika eneo la shule.

Utapata wanakanyaga haya maua au kung’oa baadhi ya miti iliyopandwa. Hii ni hali ya kukosa kuelewa kuwa mimea hutusaidia kwa njia nyingi. Ni vyema kupita katika maeneo yaliyotengwa kuwa njia badala ya kuzikanyaga zile nyasi ambazo hupatia shule rangi nzuri ya kijani kibichi.

Vyoo vya shule vinahitaji kuwa na usafi wa hali ya juu kwa kuoshwa mara kwa mara. Wanafunzi wengi wanapoambiwa waoshe vyoo huona kama wamedharauliwa kutekeleza jukumu hilo bila kujua kuwa huo ni wajibu wao. Hata wengine hujisaidia kwa kuchafua kuta au sakafu bila kulenga eneo linalofaa. Nzi wanaovutiwa na uchafu huu huweza kusababishia binadamu maradhi na hatimaye vifo.

Hata zile taka zikitapakazwa shuleni na baadhi ya wanafunzi wasiojali, hufanya shule iwe na mazingira mabaya. Utafunaji wa miwa na kutupwa kwa maganda yake shuleni haifai. Hata taka zenyewe zinafaa kukusanywa na kutupwa kwenye jalala au sehemu iliyotengwa.

Kijumla, mazingira yetu yanafaa kutunzwa vizuri. Ni wajibu wa wanafunzi wote shuleni kuhakikisha kuwa suala la usafi linashughulikiwa. Hawafai kuliachia tu walimu wao au viranja wao.

2. Shirikiana katika kujibu maswali yafuatayo;

(a) Kwa nini ni muhimu kwa mwanafunzi kuhifadhi mazingira ya shule.

(b) Uhusiano wa wanafunzi wanaoharibu mazingira na walimu wao huwa vipi kulingana na taarifa.

(c) Elezeni njia zozote tano ambazo wanafunzi hupitia kuharibu mazingira ya shuleni kulingana na kifungu ulichosoma.

(d) Kwa nini ni muhimu kutunza; i) mimea ii) vyoo

(e) Tajeni maeneo mbalimbali ya shule yanayostahili kutunzwa kulingana na taarifa uliyosoma.

Funzo f: Sarufi: Ukanushaji wa sentensi

Stadi: Kusoma na kuandika

Shughuli 7.6: Kutambua ukanushaji wa sentensi katika ngeli mbalimbali.

Katika vikundi,

1. Shirikiana katika kusoma jozi za sentensi; moja yakinifu na nyingine iliyokanushwa kisha mtambue na kujadili viambishi ambavyo vimetumiwa kukanushwa.

Funzo g: Sarufi: Usemi halisi na usemi wa taarifa

Stadi: Kusoma na kuandika

Shughuli 7.7: Kutunga sentensi katika usemi halisi na usemi wa taarifa.

Katika vikundi,

1. Rejeleeni shughuli 1.6 katika kitabu hiki kisha mshirikiane katika kutambua matumizi ya usemi halisi na usemi wa taarifa katika sentensi.

2. Mkiwa wawili wawili, someni kifungu kifuatacho huku mkitambua usemi halisi na usemi wa taarifa.

Juma alimweleza Musa, “Ukataji wa miti bila mpango hunikasirisha sana”. Musa alisikiliza maelezo haya kwa makini kisha akamjibu, “Hilo linakukasirisha wewe! Mimi hukasirishwa sana na uchimbaji wa migodi, kutafuta madini bila ruhusa ya serikali. Sipendi mashimo haya yakiachwa. Huwa hatari kwa maisha ya binadamu”.

Musa aliyevutiwa na usemaji wa Juma alienda nyumbani akaripotia babake kwa kusema kwamba ukataji wa miti bila mpango humkasirisha Juma. Babake Musa hatimaye alimwagiza, “Nenda ukawapeleke mifugo malishoni”. Naye Musa akamwuliza, “Je, baba ungependa nikae malishoni hadi saa ngapi?”. “Hakikisha unarudi saa kumi na mbili jioni”. Babake Musa alijibu. Musa alitoka hapo akamchukua nduguye waende malishoni. Alimwelezea kwamba baba yao alitaka wahakikishe wanarudi saa kumi na mbili za jioni.

3. Mkiwa wawili wawili, mwelezee mwenzako maana ya usemi halisi na usemi wa taarifa kwa kurejelea kifungu hicho mlichosoma.

4. Kwa kurejelea kifungu mlichosoma, shirikiana katika kuweka maneno au sentensi za usemi halisi za wahusika wafuatao katika usemi wa taarifa:

(a) Juma

(b) Musa

5. Tungeni sentensi zozote angalau kumi katika usemi halisi na kuzigeuza katika usemi wa taarifa.

Funzo h: Fasihi simulizi

Stadi: Kusikiliza, kuzungumza na kuandika

Shughuli 7.8: Kutaja na kueleza istiari na tashbihi mbalimbali.

i) Istiari

1. Mkiwa wawili wawili, tafuteni na kujadili maana ya istiari.

2. Tumia ‘ni’ kulinganisha moja kwa moja hali, sifa au tabia ya binadamu na ya kiumbe au kitu katika michoro kisha ueleze maana yake.

Kwa mfano;

Mafene ni ndovu.

Maana: Mafene ni mnene sana.

3. Shirikiana katika kutunga sentensi za istiari na kisha mtaje sifa au tabia kutokana na istiari hizo.

4. Elezeni maana ya istiari zifuatazo:

(a) Yeye ni kondoo.

(b) Msichana huyu ni kinyonga.

(c) Kijana huyo ni chiriku.

(d) Huyo ni sabuni yake ya roho.

(e) Watoto huwa ni mzigo.

(f) Wazee ni ngao ya jamii.

(g) Dunia ni duara.

(h) Mwana huyu ni macho yetu.

ii) Tashbihi

1. Mkiwa wawili wawili, tafuteni na kujadili maana ya neno tashbihi.

2. Tumieni neno ‘kama’ au ‘sawa na’ au ‘mithili ya’ kulinganisha sifa au tabia fulani na kiumbe katika picha au mchoro.

Kwa mfano;

Msichana huyu ni mrembo kama Malaika.

3. Tungeni sentensi angalau kumi zenye matumizi ya tashbihi.

4. Kamilisheni tashbihi zifuatazo kwa njia ifaayo:

(a) Mchafu kama…

(b) Anaenda kasi kama …

(c) Ana shingo ndefu kama…

(d) Ana miguu mirefu kama …

(e) ……… kama wembe.

(f) . …………. kama maji mtungini

(g) …….. kama nguruwe.

Funzo i: Insha: Utaratibu wa kuandika barua rasmi na tawasifu

Stadi: Kusoma na kuandika

Shughuli 7.9: Kueleza utaratibu wa kuandika barua rasmi na tawasifu.

Katika vikundi,

Someni vifungu vya barua rasmi na wasifukazi vilivyoambatanishwa hapa chini kisha jadilini katika vikundi vyenu vipengele mbalimbali vya miundo iliyotumiwa kuviandika.

Shule ya Upili ya Dokolo,

Sanduku la Posta 400,

Dokolo.

16-07-2024.

Mkurugenzi,

Gazeti la The New Vision,

Sanduku la Posta 9815,

Kampala.

Kwa Bi/Bw,

KUH: KAZI YA UANDISHI WA HABARI

Kutokana na tangazo katika gazeti lenu la The New Vision la tarehe 12.06.2024 kuwa mnahitaji waandishi wa habari wa nyanja tofautitofauti, ningependa kuwasilisha ombi langu kama nilivyodokeza kwenye mintarafu hapa juu.

Mimi ni Mwanauganda wa jinsia ya kiume. Nina umri wa miaka ishirini na sita kutoka mkoa wa Kasikazini. Nimesoma masomo ya shule na kuhitimu vizuri kidato cha sita mwaka wa 2018. Aidha mimi ni mhitimu wa taaluma ya Uanahabari kutoka Chuo Kikuu cha Gulu. Pia nina tajriba ya kazi hii ambapo nimefanyia vyombo kadhaa vya habari kama ripota wa kibinafsi.

Habari zaidi kunihusu zinaweza kurejelewa kutoka wasifukazi wangu ulioambatanishwa na barua hii.

Ninaamini mtanipa nafasi hii ili niweze kuwaletea habari kuhusu uwanja ninaopenda wa mazingira kutoka eneo hili au kokote mtakaponituma nchini.

Asante sana.

Wako mwaminifu

PNssubuga

Peterson Nsubuga Oboi.

WAREJELEWA

1. Bi. Mutenyo Wafula,

Chuo Kikuu cha Gulu S.L.P 360,

Gulu Rununu: +256701303303.

2. Bw. Rwenkuba Nathan

Mwalimu Mkuu

Shule ya Upili ya Daraja ya juu ya Dokolo,

S.L.P. 345 Dokolo.

+256776667667.

Funzo j: Insha: Barua rasmi

Stadi: Kuandika

Shughuli 7.10: Kuandika barua rasmi na tawasifu.

Katika vikundi;

Andikeni barua rasmi pamoja na wasifukazi kwa meneja mkiomba kazi katika kiwanda cha uchimbaji madini kinachopatikana wilayani Kasese au cha mafuta kinachopatikana wilayani Hoima.

Muhtasari wa matarajio ya mada

Katika mada hii, umejifunza: kutambua msamiati wa madini mbalimbali. kueleza umuhimu wa rasilimali kufafanua hatua mbalimbali za kutunza mazingira. kudhihirisha upandaji wa miti ili kutunza mazingira. kusoma makala yanayohusu uharibifu wa mazingira. kutambua na kubaini ukanushaji wa sentensi katika ngeli tofauti. kugeuza misemo na sentensi halisi kuwa za taarifa. kutaja na kuelezea istiari na tashbihi. kueleza utaratibu wa kuandika barua rasmi na wasifukazi. kuandika barua rasmi.

Assignment

Mfano wa Shughuli jumlishi: Rasilimali

ASSIGNMENT : Mfano wa Shughuli jumlishi: Rasilimali MARKS : 10  DURATION : 1 week, 3 days

 

Courses

Featured Downloads